Tuesday, November 12, 2013

Uchunguzi Kompyuta ya Mvungi kiza Kinene

Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, akiwaonyesha waandishi wa habari (hawapo pichani), mapanga matano yanayodaiwa kutumika kumjeruhi Dk. Sengondo Mvungi, baada ya kuvamiwa nyumbani kwake eneo la Kibamba, nje kidogo ya Jiji la Dares Salaam na wanaosadikiwa kuwa majambazi. Wa pili kulia ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi.(PICHA: OMAR FUNGO)
Jeshi la Polisi limetangaza kuongezeka kwa watuhumiwa wa tukio la kuvamiwa na kujeruhiwa vibaya kwa Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Dk. Sengondo Mvungi, bila kueleza kompyuta mpakato (laptop) yake aliyoporwa kama imepatikana ama la.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk. Emmanuel Nchimbi, na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, walizungumza na waandishi wa habari jana kuelezea mwenendo wa upelelezi wa tukio hilo huku wakisema watuhumiwa watatu zaidi wametiwa mbaroni.

Waziri Nchimbi alisema upelelezi umefikia asilimia 80 na watuhumiwa tisa wamekwisha kukamatwa na vielelezo mbalimbali. Kabla ya jana, Jeshi hili lilitangaza kukamata watuhumiwa sita.

Kova aliwataja watuhumiwa na vielelezo walivyokamatwa navyo kuwa ni mapanga matano na simu aina ya Nokia iliyoporwa nyumbani kwa Dk. Mvungi.

Hata hivyo, Dk. Nchimbi na Kova walisema upelelezi wa kina unaendelea juu ya kompyuta ya Dk. Mvungi na kwamba baada ya muda mfupi taarifa kamili itatolewa.

Dk. Mvungi ambaye ni mwanasheria mkongwe aliyebobea katika masuala ya sheria na katiba, alihamishiwa Afrika Kusini kwa matibabu zaidi.

Kuna hisia kwa baadhi ya watu kwamba huenda alifavamiwa nyumbani kwake kwa hisia kuwa wajumbe wa tume hiyo wanalipwa fedha nyingi na hivyo kulikuwa na uwezekano wa kuwa na fedha nyingi nyumbani kwake.

Hata hivyo, pamoja na hisia hizo, pia kuna hofu miongoni mwa jamii kuwa huenda alijeruhiwa na kuporwa laptop yake ambayo ilikuwa na taarifa muhimu na nyeti kuhusu mchakato mzima wa Katiba Mpya na taarifa hizo zitakuwa mikononi mwa watu wasiostahili.

Hofu hiyo inatokana na ukweli kwamba miongoni mwa vitu vilivyoporwa nyumbani kwa Dk. Mvungi, Mbezi Msakuzi baada ya kupigwa mapanga na majambazi hao ni laptop ambayo ni moja ya nyenzo zake muhimu za kazi.

Hofu hii inaelezwa kutanda ndani ya Tume kwa kuwa mbali ya kuwako na uwezekano huo, kwa kuwa Dk. Mvungi amebobea katika masuala ya katiba alikuwa nguzo muhimu kwa Tume hasa katika kipindi hiki cha mwisho cha kuandaa rasimu ya mwisho ya Katiba Mpya.

Katika mkutano wa jana, Dk. Nchimbi alisema Jeshi la Polisi kupitia kitengo cha intelijensia lilifanikiwa kuwakamata wahalifu hao ambao walionyesha vifaa walivyotumia ambavyo ni mapanga matano na kigoda kimoja.

Dk. Nchimbi alisema kwa asilimia 80 upelelezi wa tukio hilo umekamilika kwa watumuhumiwa na vilelezo muhimu vimepatikana na wakati wowote watafikishwa mahakamani.

Kamanda Kova alidai kuwa watuhumiwa hao ni Msigwa Mpopela (30) kwa jina maarufu Matonya mkazi wa Vingunguti na ambaye kabla ya tukio alikuwa fundi ujenzi nyumbani kwa Dk. Mvungi.

Alidai Mpopela na mtuhumiwa mwingine Chabago Magozi ndiyo vinara wa uhalifu huo na kwamba baada ya kukamatwa walitaja wenzao na silaha walizotumia na kukamatwa na simu aina ya Nokia ambayo iliporwa nyumbani kwa Dk. Mvungi.

Wengine ni Ahemed Ally (40) maarufu kama Khatibu mkazi wa Mwananyamala; Zakaria Rafael Masesa (25), mkazi wa Buguruni Mlapa ambaye ni dereva bodaboda na Longushi Semaliko Losingo (29), mfanyabashara wa ugoro mkazi wa Msimbazi.

Wengine ni Paul Yamusi (29), Juma Hamisi (29) maarufu Kangua Mnanda Saluwa (40) kwa jina maarufu White au Mlewa wote wakazi wa Vingunguti.

Kova alisema jalada la kesi iliyo limefikishwa kwa mwanasheria wa serikali ili kuona kama kuna kesi dhidi yao na kuwa ikibainika watafikishwa mahakamani.

Aidha, alisema watuhumiwa hao walikamatwa kwa haraka kutokana na ushirikiano kutoka familia ya Dk. Mvungi na vyombo vya habari kutoandika sana.

Dk. Mvungi, aliyewahi kuwa Mhadhiri Mwandamizi Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alipatwa na mkasa huo usiku wa kuamkia Novemba 4, mwaka huu nyumbani kwake Mbezi Msakuzi, Manispaa ya Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
CHANZO: NIPASHE