Friday, January 31, 2014

SAMATTA MCHEZAJI BORA WA MWAKA TP MAZEMBE


Samata-Bwana58021_6e83d.jpg
 
MBWANA Ally Samatta ameshinda tuzo ya mchezaji bora wa mwaka 2013 wa klabu ya Tout Puissant Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
 
Mshambuliaji huyo wa Tanzania, maarufu kama Sama Goal amewashinda Solomon Asante na Robert Kidiaba alioingia fainali.
 
Samatta alipata kura 248, Asante Solomon kura 219, Robert Kidiaba kura 200, Nathan Sinkala kura 97 na Rainford Kalaba kura 67.
 
Mafanikio hayo yametokana na Samatta kuwa tegemeo la mabao la Mazembe kuanzia Ligi Kuu ya DRC, Ligi ya Mabingwa na baadaye Kombe la Shirikisho, ambako timu hiyo ilifika fainali. Mazembe inaye Mtanzania mwingine, Thomas Ulimwengu

source: mjengwa blog

Wednesday, January 29, 2014

Neno Fupi La Usiku: Fimbo Ya Mussa...


Ndugu zangu,
Inasemwa, kuwa Mungu alimuuliza Mussa; " Umeshika nini mkononi?"
Naye Mussa akajibu; " E baba, nimeshika fimbo tu!"
Mungu akamwambia Mussa;
" Yatosha sana kuwakombolea Wana-Israel kutoka kwenye nchi ya Misri"
Na hakika, kwa mwanadamu, kila ulichonacho mkononi chatosha kabisa kufanya makubwa maishani mwako.
Yumkini wengine hatuna fedha mifukoni za kutosha kugawa kwa wengine wenye kuhitaji, lakini, na tuamini, kuwa hata yale machache tuliyonayo vichwani mwetu, yatosha kabisa kuwakomboa wanadamu wenzetu wenye kutaabika na waliozama kwenye lindi la umasikini.
Ni Neno Fupi La Usiku. ( Pichani nikizungumza na akina mama wa umoja wa wakulima na wajasiri amali Mbarali, ujulikanao kama UWAKIUMBA, Chimala, Leo asubuhi.)
Maggid Mjengwa,
Iringa.

Monday, January 27, 2014

Dk Lwaitama ashushwa kwenye ndege ya PrecisionAir alipohoji ni kwa nini asipewe maelekezo katika lugha ya Kiswahili

Ifuatayo ni nukuu ya taarifa aliyoiandika Ndimara Tegambwage jana Jumapili, Januari 26, 2013...
Dk. Lwaitama atolewa kwenye ndege, akamatwa na polisi Mwanza

Niliongea na Dk. Azaveli Lwaitama akiwa Mwanza baada ya kuandika maelezo yake kwenye kituo cha polisi cha uwanja wa ndege Mwanza na kuachiwa kwa kilichoitwa "dhamana ya polisi." Anatakiwa kuripoti polisi uwanjani hapo kesho asubuhi kuona iwapo polisi wameamua kumfikisha mahakamani. Nasimulia alivyonisimulia.

Dk. Lwaitama alitoka Dar es Salaam leo asubuhi. Akatua Mwanza. Alikuwa anakwenda Bukoba. Alipanda ndege ya kampuni ileile iliyomtoa Dar es Salaam leo hii - PrecisionAir. Hii ya kwenda Bukoba ilikuwa Na. PW 0492. Alikwenda hadi kwenye kiti chake Na. 2B. Hapa ndipo kuna milango ya dharura kwa pande zote mbili za ndege - kulia na kushoto.

Ndipo akaja mfanyakazi wa ndege. Akamuuliza iwapo anajua Kiingereza. Baada ya mzaha wa kawaida katika kuuliza iwapo 
ni lazima kujua Kiingereza, ndipo mfanyakazi akamwambia kuwa kama hajui lugha hiyo basi ahame kiti na kukaa kwingine kwani kuna maelezo rasmi ambayo yanatolewa kwa "lugha ya anga" - Aviation Language.

Ilikuwa katika kujibizana kwa nini lugha ya anga isiwe lugha ambayo abiria wengi wanaelewa - huku Dk. Lwaitama akisema katika ndege nyingi alizosafiri kote duniani alikokwenda, lugha za anga huwa zile za wasafiri wengi wa eneo husika na lugha nyingine za kimataifa; huku akishauri kuwa maelezo yangekuwa kwa Kiswahili na Kiingereza - ndipo mhudumu alikimbilia mwenzake ambaye naye hakutaka kumsikiliza Lwaitama na wote wawili wakakimbilia kwa chumba cha rubani kushitaki kuwa kuna mtu "anafanya fujo." Tayari Dk. Lwaitama akawa abiria "hatari."

Rubani hakutaka kusikiliza abiria wake anasema nini; hakumuuliza hata mwenzake waliokaa pamoja juu ya fujo alizoripotiwa; alimwambia hawezi kusafiri. Akaita polisi ambao pia hawakuuliza lolote juu ya fujo zake bali walifanya kazi moja ya kumtoa nje mkukuku.

Ni rafiki yake aliyemwita Diallo na mwanaharakati Sungusia ambao anasema aliwapigia simu wampelekee mawakili ili aweze kuandika maelezo yake mbele yao. Mawakili walifika na yeye kuadika maelezo. Mizigo yake imepelekwa Bukoba. Yeye amebaki Mwanza na kompyuta yake ndogo ya mkononi.

Dk. Lwaitama anasema, "Sina mgogoro na kampuni ya PrescisionAir, bali wahudumu ambao hawataki hata kupata maoni ya abiria. Kwanza, walipata bahati ya kuona mtu anahiari maoni moja kwa moja. Pili, kama wanafanya kazi kwenye ndege watakuwa wamesafiri katika ndege za wengine ambako niliyokuwa nayasema ni maneno na vitendo vya kawaida. Sasa fujo ni nini katika hili?

Mwalimu huyo mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema, "Hata polisi ni wa kushangaza. Mtu anakwambia huyu kafanya fujo, wewe huulizi ni fujo gani. Unambeba tu mzegamzege. Sidhani kama huu nao ni utendaji bora katika nchi iliyohuru; ambako polisi wanapaswa kuwa na utulivu wa akili na kufanya kazi kwa kufikiri kuliko kwa kuambiwa tu."

Dk. Lwaitana anaamkia kituo cha polisi uwanja wa ndege kesho asubuhi kuambiwa "uamuzi wa polisi."

Haikufahamika iwapo mhudumu wa ndege mswahili, aliyekuwa anaongea Kiswahili, hakuwa na tafsiri ya maneno ya Kiingereza ambayo alitaka kumwambia abiria wake.

ndimara.

Utekaji malori wasababisha maelfu kukwama Nzega


nzegaclip_0b537.jpg

Nzega. Zaidi ya magari 1,000 yamekwama kwenye Barabara Kuu ya Mwanza - Dar es Salaam katika Kijiji cha Ngonho, Kata ya Miguwa, wilayani Nzega, kutokana utekaji wa malori uliofanywa juzi usiku. (JM)

Kutokana na tukio hilo, waligoma kuondoa magari yao na kusababisha mabasi ya abiria na malori ya mizigo kukwama wakati abiria wapatao 3,000 wakitaabika kwa kukosa chakula na maji.

Madereva hao waligoma kuondoa magari yao baada ya kukasirishwa na kitendo cha polisi wa Nzega kushindwa kuwasaidia wakati walipotekwa.

Madereva hao wameapa kutoondoa magari hayo hadi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, Waziri wa Mambo ya Ndani, Mathias Chikawe au Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Fatma Mwassa watakapofika kwenye eneo hilo ili kusikiliza kilio chao.
Unyama wa watekaji

Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya ya Nzega, Emmanuel Mihayo alisema watu walijeruhiwa vibaya kwenye utekaji huo kwa kukatwa masikio na kutobolewa macho.

Dk Mihayo aliwataja majeruhi hao kuwa ni raia wa Burundi, Herelina Eddy, ambaye alitobolewa macho na hali yake ilikuwa mbaya na alikuwa kwenye maandalizi ya kupelekwa Hospitali ya Rufaa ya Nkinga kwa matibabu zaidi.

Alisema majeruhi wengine wawili wanaendelea vizuri na matibabu katika hospitali hiyo. Majeruhi hao ni Abraham Ismail na Omary Adrian, ambao wote ni wakazi wa Dar es Salaam.

Alisema Adrian alikatwa sikio na shavu pamoja na mkono wa kushoto wakati Ismail alijeruhiwa sehemu mbalimbali za mwili.
Polisi watuhumiwa

Mmoja wa madereva waliotekwa, ambaye aliomba jina lake kuhifadhiwa alisema kuwa polisi wa Nzega waliombwa kutoa msaada lakini walikataa. CHANZO 

MWANANCHI

Saturday, January 25, 2014

AJALI YA NDEGE PEMBA

Picture
Ndege ya shirika la Zan Air imeanguka Pemba jioni hii ikiwa imebeba jumla ya abiria 19, miongoni mwa abiria hao pia alikuwamo Waziri wa Habari na Katiba wa Zanzibar, Mhe. Abubakar Khamis. Abiria wote wametoka salama. (picha, maelezo: SufianiMafoto blog