Monday, January 14, 2013

AFANDE SELE: NANI ATABAKI MIKOANI??? KAMA KILA KITU KIPO DAR ES SALAAM



Na Selemani Msindi 'Afande Sele', Morogoro

Wanalalamika kila siku Chinga kukimbilia Dar-es-Salaam na ongezeko la watu dsm, foleni halafu bado kila kitu wanataka walundike Dsm. Sasa nani atabaki Mikoani? Afanye nini Lindi, Mtwara, Kigoma, Shinyanga, Iringa, Singida, Mara n.k kama kila kitu kipo Dsm?

Ukistajabu ya Musa .... Kila siku viongozi wa Serikali wanalalamika kwamba wamachinga/vijana mikoani kukimbilia DSM ni tatizo la kitaifa au ni bomu hatari kwa amani ya Taifa, ila kila siku wanajenga na kubomoa miundo mbinu ya Jiji la Dsm ili kukabiliana na foleni, misongamano ya watu na makazi kwa kuwa ongezeko la watu Dsm linakua maradufu kila mwaka na yote ni kwa sababu nyanja kuu za ajira/uchumi kwa kiasi kikubwa zipo Dsm. Watu wengi huja Dsm sasa kitu cha ajabu;

Bado viongozi wa Serikali tena Wasomi wakubwa (Maprofesa/madokta) hawalioni hilo tatizo kama ni tatizo ambalo hata asiejua kusoma/kuandika analiona lakini wao hawaoni wanazidi kulazimisha kila kitu kiwe DSM, nani atabaki Kigoma, Lindi, Mtwara, Singida n.k afanye nini?

Cha ajabu wanawabeza wananchi wa Lindi na Mtwara ni wapuuzi/wahaini wa kupuuzwa wajinga wasiojielewa kwa kukosa shukrani, eti wamepewa umeme wa megawati 18, hawawezi kuutumia kwa lolote, watautumia ikiwa mumeua viwanda vya Korosho Lindi na Mtwara, Mumeua Mashamba ya Mkonge Lindi, Karanga Nachingwea, mnawakopa Korosho na Ufuta hamuwalipi kwa wakati, hawapati pembejeo za kilimo kama inavyostahili, ni dhambi kubwa kuwaita wapuuzi, hawakatai Umeme unaotokana na Gesi ya kusini kutumika Tanzania nzima! 

Ndani ya Miaka 50 ya Uhuru mmeshindwa kuwawekea barabara mpaka leo inasuasua haijaisha ni kama km 500 tu, Mnajua kuzorota kwa uchumi wa mikoa ya Kusini ni kutokana na kutumika kwake kwenye Ukombozi wa Nchi za kusini mwa Afrika! Msumbiji, South Afrika, Angola n.k.. Katika mwaka wa uchumi unaoishia Novemba Korosho imeingizi Dola za Kimarekani Milioni 151, pamba dola za kimarekani Milioni 53... licha ya zao la korosho kuliingizia taifa kiasi cha shilingi trilioni 7.2, ndiyo mikoa iliyo nyuma kimaendeleo katika miaka 51 ya uhuru.

MUNGU IBARIKI TANZANIA

source habari na matukio blog

No comments:

Post a Comment