Tuesday, April 29, 2014

Ushirikiano huu wa ‘Ukawa’ uwe endelevu

mboye_a034a.jpg
Bila shaka kila mwananchi anayeitakia mema nchi yetu amevutiwa na habari zilizochapishwa katika gazeti hili jana kwamba vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), vimeamua kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani.
Viongozi wakuu wa vyama hivyo tayari wamekubaliana kuanza mchakato huo na wameandika mapendekezo na kuyapeleka katika sekretarieti za vyama vyao kwa ajili ya kufanyiwa uchambuzi.
Sisi tunaona kitendo hicho cha vyama vinavyounda Ukawa kuwa ni hatua muhimu ya kuongeza nguvu ili kuongeza ushindani ambao ni muhimu katika mustakabali wa nchi yetu kisiasa na hivyo kusaidia nyanja nyingine za kiuchumi na kijamii.
Tangu kuruhusiwa tena kwa siasa huru karibu miaka 22 sasa, bado nchi haijashuhudia ushindani wa kweli unaoweza kuwafanya watawala kuwajibika kwa wananchi kutokana na kuona hatari ya kuondolewa madarakani na vyama pinzani.
Hii imetokana na vyama shindani katika siasa kukumbwa na mifarakano ya kisiasa ambayo imekuwa ikiwagawa na hivyo kuingia kwenye chaguzi vikiwa dhaifu na hivyo kushindwa vibaya na chama tawala na matokeo yake yamekuwa ni wananchi wengi kukata tamaa na hivyo kusababisha idadi ya wanaoshiriki kupiga kura kupungua mwaka hadi mwaka kutokana na kutoona faida ya siasa za ushindani.
Pengine hiyo ndiyo sababu iliyofanya wananchi wapendekeze kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba vyama viruhusiwe kuunganisha nguvu wakati wa chaguzi kwa kuwa wameona bila ya nguvu ya vyama shindani, watawala wawataendelea kuongoza kwa mazoea na matokeo yake ni wananchi kuendelea na umaskini wao na kuona uhuru wa vyama vya kisiasa hausaidii kuwa kuboresha maisha yao.
Si nia yetu kuona chama tawala kikiondolewa madarakani na vyama shindani, lakini tunachotaka kuona na ushindani wa dhati, makini na wa kweli ambao, kwa taifa lolote lile, ni afya kwa ustawi wa wa taifa kwa kuwa huongeza uwajibikaji kwa watawala.
Hakuna ubishi kwamba upinzani wenye nguvu huisukuma serikali ichape kazi na kuwatumikia wananchi kwa kutambua kwamba ikiboronga itaondolewa madarakani na serikali kivuli ambayo ni vyama vya upinzani.
Vyama legelege vya upinzani huogopa kivuli cha serikali na kufifisha maendeleo na kuzima matumaini ya wananchi wanaotaka kuona uwajibikaji serikalini, kwani huwa chachu ya kuendeleza tawala za kiimla zisizothamini demokrasia na zisizowajibika kwa wananchi.
Ndiyo maana tunawapongeza viongozi wa Ukawa kwa kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu na kuwa wamoja ili kuweka ushindani wa kweli katika mazingira ya kisiasa tuliyomo.
Tunachoweza kuwashauri viongozi wa Ukawa ni kuwa makini na kuondoa tofauti zinazowatenganisha. Ukawa isitarajie kwamba kila kitu kitakuwa mteremko, kwani bado sheria kandamizi ambazo zimekuwa zikikwaza shughuli za upinzani bado hazijafutwa.
Ni matarajio yetu kwamba serikali na chama tawala kitachukulia hatua hiyo ya Ukawa kuwa changamoto ya kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi na si kuanza kujenga chuki na kutafuta mbinu za kuikwamisha
Serikali haina budi kuhakikisha kuwa vyama vyote vinapewa nafasi sawa ya ushindani na kujengewa mazingira ya kukua ili kukifanya chama chochote kinachopewa madaraka kiwajibike kwa wananchi na kuwaletea maendeleo.(E.L)

source: mjengwa blog

Breaking News: Azam FC wakamilisha usajili wa Kavumbagu


KAVUMBAGUNEW_43297.jpg
Klabu ya Azam FC imeanza rasmi maandalizi ya kutetea ubingwa wao msimu ujao na michuano ya kimataifa kwa kukamilisha usajili wa mchezaji wa kimataifa wa Burundi aliyekuwa anakipiga kwenye klabu ya Yanga.
Taarifa rasmi zilizothibitishwa na meneja wa Azam FC Jemedari Said ni kwamba mshambuliaji Didier Kavumbagu amejiunga na klabu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja.
“Ni kweli Kavumbagu tumemalizana nae na amesaini mkataba wa mwaka mmoja. Taarifa zaidi zitatolewa baadae.” Alikaririwa Jemedari.
Kavumbagu alitua nchini Tanzania akitokea Burundi alipokuwa anaitumikia Vital O na kuja kujiunga na Yanga misimu miwili iliyopita.(Awadh Ibrahim)
 
source: mjengwa blog

Basi la Hood lilivyoungua moto na kuteketea kabisa



Zaidi ya Abiria 55 waliokuwa ndani ya Basi la kampuni ya Hood, wakisafiri kutoka Mbeya kwenda Arusha walinusurika kufa baada ya Basi hilo kushika moto na kuteketea kabisa katika kijiji cha Kilolele-Chalinze Mkoani Pwani.Chanzo: http://bit.ly/1m4F9cG (J M)

source: mjengwa blog

Sunday, April 27, 2014

Sherehe zatikisa Dar

  Makomandoo wa jeshi wawa kivutio
  Askari wa Miavuli wapongezwa
  Wapinzani wasusia Sherehe
Askari wa miavuli akishuka na parachuti kwenye Uwanja wa Uhruru wakati wa sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar jijini Dar es Salaam jana.
Sherehe za miaka 50 ya Muungano jana zilifana na kusababisha viwanja vya Uhuru na Taifa kufurika umati wa watu waliojitokeza kuungana na viongozi wa kitaifa na kimataifa kusherehekea maadhimisho hayo.
Uwanja wa Uhuru ambao ulitengwa kutumika kwa ajili ya sherehe hizo, baada ya kujaa askari walilazimika kufungua lango kuu la kuingilia Uwanja wa Taifa, ili wananchi waliokuwa nje waingie kushuhudia yaliyokuwa yakiendelea uwanja wa Uhuru.

Wananchi wengine walilazimika kukaa nje ili kufuatilia sherehei za Muungano kupitia televisheni iliyokuwa imefungwa nje ya viwanja.

Mageti ya uwanja wa Uhuru yalikuwa wazi kuanzia saa 12:30 asubuhi na ilipofikia saa 2:30 viongozi mbalimbali wa ngazi tofauti ndani na nje ya nchi walianza kuingia.

Sherehe hizo  zilihudhuriwa na marais sita wa kimataifa, akiwemo Mfalme wa Lesotho Letsie III, Mfamle wa Swaziland Mswati III,  Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Burundi,  Pierre Nkurunzinza, Rais wa Malawi, Joyce Banda na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Pia zilihudhuriwa na marais wastaafu wa ndani na nje ya nchi akiwemo Sam Nujoma (Namibia), Rupia Banda (Zambia) na Mwai Kibaki (Kenya).

Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria sherehe hizo.

Wawakilishi wa nchi, mashirika ya kimataifa pamoja na mabalozi na viongozi wengine wa kitaifa waliohudhuria ni Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Amir Kificho na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman  Kinana.

Pia maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi za Oman , Angola, Kuwait, Mauritius, Botswana, Ghana, Jamaica, Ufaransa , Korea Kusini, Brazil, Uholanzi, Finland Uingereza, Qatar, Eritrea, Misri na Algeria.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani walionekana kususia sherehe hizo kwa kutoonekana uwanjani hapo.

Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,  Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambao wanaunda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Viongozi ambao walianza ni Spika wa Bunge, Anne Makinda akifuatiwa na makatibu wakuu, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Abeid Karume, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa  kisha akafuatia mke wa marehemu Abeid Karume, Fatma.

Haikupita muda, aliingia  Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, balozi Seif Ali Iddi, na kufuatiwa na makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad,  jukwaa kuu eneo walikokaa mawaziri na wabunge, walisikika wakisema, mbili yatosha tatu ya nini, CCM yatosha.

Ilipotimu saa 3:20 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwasili akifuatiwa na mawaziri kutoka nchi mbalimbali kisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliingia.

Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal kisha Rais Mstaafu wa Kenya, Mwaki Kibaki kisha saa 3:48 aliingia Uhuru Kenyatta na Rais Uganda, Yoweri Museven.

Baada ya viongozi hao wa kimataifa kuingia, Rais Jakaya Kikwete aliwasili saa 4:20 asubuhi akiwa kwenye gari maalum la wazi na kupokelewa na vifijo na nderemo na wananchi waliokuwa uwanjani hapo.

Rais Kikwete akiwa kwenye msafara uliokuwa na magari matano na pikipiki 24 alizunguka uwanja huku halaiki ya watu ikimpokea kwa kunyoosha kofia na bendera ya taifa juu.

Baadaye, alipanda kwenye jukwaa dogo ambapo mizinga 21 ilipigwa ikiwa ni heshima kwa Rais na kufuatiwa na wimbo wa taifa.

Alikagua gwaride na baadaye maonyesho ya kijeshi yalianza na kutoa nafasi kwa Rais Kikwete na viongozi wengine kushuhudia mazoezi ya askari waendao kwa miguu, anga na majini.

Wanajeshi hao walionyesha zana mbalimbali za kivita zitumiwazo na askari waendao kwa miguu ambapo walipitisha magari mbele ya Rais.

Vilevile, askari watano wa miamvuli walionyesha umahiri wao wa kuruka (Troop Commander) kutoka ndani ya ndege ya kivita kisha kuelea angani umbali wa futi 4,500 kutoka usawa wa bahari na baadaye kutua ardhini.

Kikosi hicho kiliongozwa na Luteni Joseph Kabipe na kuwa kivutuo kikubwa na kusababisha Rais kukiita mbele na kukipongeza kwa kuwapa mikono.

Onyesho lingine lililovutia watu ni la makamandoo wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) linaloongozwa na Luteni Utawangu  ambao walionyesha umahiri wa kupambana na adui kwa kutumia mikono.

Pia jeshi la Magereza lilionyesha mbinu mbalimbali za kukabiliana na uhalifu magerezani  huku jeshi la polisi vikosi vya mbwa na farasi vikionyesha jinsi ya kumkamata mtuhumiwa. 

Sherehe hizo zilibeba kauli mbiu isemayo, Utanzania wetu, ni Muungano wetu, tuulinde, tuuimarishe na kuudumisha.

WAZIMIA
Watu zaidi ya 70  wakiwemo watoto chini ya umri wa miaka 15 walidondoka kutokana na mshituko uliosababishwa na milio ya mizinga iliyolipuliwa viwanjani hapo.

Pia miongoni mwao walidondoka kutokana na njaa, kusimama muda mrefu  na wengine magonjwa.

Msimamizi wa huduma ya kwanza, Dk. Laurence Chipata kutoka Hospitali ya Temeke, alisema kuwa kati ya watu hao  watatu walipelekwa hopitali kwa matibabu zaidi.
Alisema wengine walipewa huduma ya kwanza na kuruhusiwa.

KIKWETE
Katika hotuba yake, Kikwete aliwaeleza nchi jirani  waishi kwa umoja, undugu na kwa upendo.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI