Sunday, April 27, 2014

Sherehe zatikisa Dar

  Makomandoo wa jeshi wawa kivutio
  Askari wa Miavuli wapongezwa
  Wapinzani wasusia Sherehe
Askari wa miavuli akishuka na parachuti kwenye Uwanja wa Uhruru wakati wa sherehe za miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar jijini Dar es Salaam jana.
Sherehe za miaka 50 ya Muungano jana zilifana na kusababisha viwanja vya Uhuru na Taifa kufurika umati wa watu waliojitokeza kuungana na viongozi wa kitaifa na kimataifa kusherehekea maadhimisho hayo.
Uwanja wa Uhuru ambao ulitengwa kutumika kwa ajili ya sherehe hizo, baada ya kujaa askari walilazimika kufungua lango kuu la kuingilia Uwanja wa Taifa, ili wananchi waliokuwa nje waingie kushuhudia yaliyokuwa yakiendelea uwanja wa Uhuru.

Wananchi wengine walilazimika kukaa nje ili kufuatilia sherehei za Muungano kupitia televisheni iliyokuwa imefungwa nje ya viwanja.

Mageti ya uwanja wa Uhuru yalikuwa wazi kuanzia saa 12:30 asubuhi na ilipofikia saa 2:30 viongozi mbalimbali wa ngazi tofauti ndani na nje ya nchi walianza kuingia.

Sherehe hizo  zilihudhuriwa na marais sita wa kimataifa, akiwemo Mfalme wa Lesotho Letsie III, Mfamle wa Swaziland Mswati III,  Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, Rais wa Burundi,  Pierre Nkurunzinza, Rais wa Malawi, Joyce Banda na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.

Pia zilihudhuriwa na marais wastaafu wa ndani na nje ya nchi akiwemo Sam Nujoma (Namibia), Rupia Banda (Zambia) na Mwai Kibaki (Kenya).

Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ni miongoni mwa viongozi waliohudhuria sherehe hizo.

Wawakilishi wa nchi, mashirika ya kimataifa pamoja na mabalozi na viongozi wengine wa kitaifa waliohudhuria ni Waziri Mkuu mstaafu Edward Lowassa, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Pandu Amir Kificho na Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahaman  Kinana.

Pia maadhimisho hayo yalihudhuriwa na wawakilishi kutoka nchi za Oman , Angola, Kuwait, Mauritius, Botswana, Ghana, Jamaica, Ufaransa , Korea Kusini, Brazil, Uholanzi, Finland Uingereza, Qatar, Eritrea, Misri na Algeria.

Hata hivyo, baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa vya upinzani walionekana kususia sherehe hizo kwa kutoonekana uwanjani hapo.

Viongozi hao ni Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe,  Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba ambao wanaunda kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA).

Viongozi ambao walianza ni Spika wa Bunge, Anne Makinda akifuatiwa na makatibu wakuu, Rais Mstaafu wa Zanzibar, Abeid Karume, Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa  kisha akafuatia mke wa marehemu Abeid Karume, Fatma.

Haikupita muda, aliingia  Makamu wa Pili wa Rais Zanzibar, balozi Seif Ali Iddi, na kufuatiwa na makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad,  jukwaa kuu eneo walikokaa mawaziri na wabunge, walisikika wakisema, mbili yatosha tatu ya nini, CCM yatosha.

Ilipotimu saa 3:20 Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliwasili akifuatiwa na mawaziri kutoka nchi mbalimbali kisha Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein aliingia.

Makamu wa Rais, Dk. Mohammed Gharib Bilal kisha Rais Mstaafu wa Kenya, Mwaki Kibaki kisha saa 3:48 aliingia Uhuru Kenyatta na Rais Uganda, Yoweri Museven.

Baada ya viongozi hao wa kimataifa kuingia, Rais Jakaya Kikwete aliwasili saa 4:20 asubuhi akiwa kwenye gari maalum la wazi na kupokelewa na vifijo na nderemo na wananchi waliokuwa uwanjani hapo.

Rais Kikwete akiwa kwenye msafara uliokuwa na magari matano na pikipiki 24 alizunguka uwanja huku halaiki ya watu ikimpokea kwa kunyoosha kofia na bendera ya taifa juu.

Baadaye, alipanda kwenye jukwaa dogo ambapo mizinga 21 ilipigwa ikiwa ni heshima kwa Rais na kufuatiwa na wimbo wa taifa.

Alikagua gwaride na baadaye maonyesho ya kijeshi yalianza na kutoa nafasi kwa Rais Kikwete na viongozi wengine kushuhudia mazoezi ya askari waendao kwa miguu, anga na majini.

Wanajeshi hao walionyesha zana mbalimbali za kivita zitumiwazo na askari waendao kwa miguu ambapo walipitisha magari mbele ya Rais.

Vilevile, askari watano wa miamvuli walionyesha umahiri wao wa kuruka (Troop Commander) kutoka ndani ya ndege ya kivita kisha kuelea angani umbali wa futi 4,500 kutoka usawa wa bahari na baadaye kutua ardhini.

Kikosi hicho kiliongozwa na Luteni Joseph Kabipe na kuwa kivutuo kikubwa na kusababisha Rais kukiita mbele na kukipongeza kwa kuwapa mikono.

Onyesho lingine lililovutia watu ni la makamandoo wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) linaloongozwa na Luteni Utawangu  ambao walionyesha umahiri wa kupambana na adui kwa kutumia mikono.

Pia jeshi la Magereza lilionyesha mbinu mbalimbali za kukabiliana na uhalifu magerezani  huku jeshi la polisi vikosi vya mbwa na farasi vikionyesha jinsi ya kumkamata mtuhumiwa. 

Sherehe hizo zilibeba kauli mbiu isemayo, Utanzania wetu, ni Muungano wetu, tuulinde, tuuimarishe na kuudumisha.

WAZIMIA
Watu zaidi ya 70  wakiwemo watoto chini ya umri wa miaka 15 walidondoka kutokana na mshituko uliosababishwa na milio ya mizinga iliyolipuliwa viwanjani hapo.

Pia miongoni mwao walidondoka kutokana na njaa, kusimama muda mrefu  na wengine magonjwa.

Msimamizi wa huduma ya kwanza, Dk. Laurence Chipata kutoka Hospitali ya Temeke, alisema kuwa kati ya watu hao  watatu walipelekwa hopitali kwa matibabu zaidi.
Alisema wengine walipewa huduma ya kwanza na kuruhusiwa.

KIKWETE
Katika hotuba yake, Kikwete aliwaeleza nchi jirani  waishi kwa umoja, undugu na kwa upendo.
 
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

No comments:

Post a Comment