Wednesday, January 2, 2013

SAJUKI KUZIKWA IJUMAA, WAZIRI FENELLA ATOA SALAMU ZA RAMBIRAMBI.


 Baadhi ya ndugu, jamaa na marafiki wakiwasili nyumbani kwa Marehemu SAJUKI Tabata Bima jijini Dar es Salaam leo.
Mke wa marehemu Wastara aliyefunikwa kanga ilikuwa ni vigumu kuamini kama mumewe kipenzi hatamuona tena alikuwa  akilia muda wote na kufarijiwa na ndugu wa karibu nyumbani kwao Tabata Bima jijini Dar. kushoto ni mama wa marehemu Bi. Zaitun

Wasanii wakiwa wamejitokeza katika msiba wa mwenzao.

Watu waliojitokeza msibani huku wengine wakiwa wamekaa kwenye mitaro ya maji.
Watu wakiwa msibani huku wakijadili mambo mbali mbali. Msiba wa Marehemu Juma Kilowoko 'Sajuki' umewagusa wengi na kuleta simanzi.
*Marehemu Juma Kilowoko anatarajiwa kuzikwa ijumaa saa 5 katika makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam

Waziri wa Habari, Vijana , Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangaraamewatumia salamu za rambirambi, ndugu, jamaa na wasanii wote nchini kufuatia kifo cha msanii Juma Kilowoko (SAJUKI) kilichotokea usiku wa kuamkia tarehe 02/01/2013 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
Taarifa iliyotolewa leo, jijini Dar es salaam ,Wizara ya Habari, Vijana na Utamauni na Michezo imepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa taarifa za kifo cha msanii huyo na kuongeza kuwa kifo hicho ni pigo katika tasnia ya filamu hapa nchini.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Kifo chake ni pengo kubwa kwa Serikali, wadau wa tasnia ya filamu na michezo ya kuigiza nchini kwa ujumla.“Nimepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha SAJUKI sina maneno ya kuelezea masikitiko na huzuni nilinayo , kwani kifo chake ni pigo katika tasnia ya filamu za michezo ya kuigiza” alisema Dkt Mukangara.

Dkt. Mukungara amewataka ndugu, jamii na wasanii wote kuwa wavumilivu na watumilivu wakati wote wa msiba na kumuombea marehemu makao mema kwa Mwenyezi Mungu.

Juma Kilowoko (SAJUKI)ni mzaliwa wa mkoa wa Ruvuma. Sajuki alianza kujihusisha na masuala ya maigizo alipojiunga na kikundi cha Kaole na baadaye filamu. Filamu alizocheza ni pamoja na Revenge ya Kampuni ya RJ.

Mwaka 2008 aliamua kuanza kutengeneza kazi zake mwenyewe ambapo filamu yake ya kwanza iitwayo Two Brothers kwa kushirikiana na Shija Deogratious ilitoka. Sajuki baadaye aliamua kuanzisha kampuni yake iitwayo WAJEY Production Company ambapo alitengeneza filamu nyingi zikiwemo Mboni Yangu, Round, Briefcase , Kijacho, Kozopata, Mchanga na Keni, 077( Zero Seven Seven).nk
Sajuki alifanikiwa kucheza michezo ya kuigiza na filamu na wasanii wengi wenye majina hapa nchini. Sajuki amebobea katika Uigizaji, Utayarishaji na Uongozaji wa filamu.

Sajuki alianza kuugua mwaka 2010 na hali ilizidi kudhoofu mwaka 2011,ambapo alikwenda kutibiwa nchini India. Wadau wengi wa tasnia ya filamu walifanikiwa kutoa michango mbalimbali iliyomwezesha Sajuki kupata matibabu yake. Alirudi na kuonekana kapata nafuu kidogo jambo ambalo lilileta matumaini na furaha kwa watanzania; aliporejea tu aliweza kutoa filamu iitwayo Kivuli huku filamu nyingine ikiwa katika hatua ya utengenezaji.

Aidha hali yake ilibadilika jambo lililolazimu alazwe katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili hadi umauti ulipomkuta usiku wa kuamkia tarehe 02/01/2013

Mungu ailaze roho ya Marehemu mahali pema peponi. AMEN.
(Picha na www.elimuboratanzania.blogspot.com

No comments:

Post a Comment