Monday, January 27, 2014

Dk Lwaitama ashushwa kwenye ndege ya PrecisionAir alipohoji ni kwa nini asipewe maelekezo katika lugha ya Kiswahili

Ifuatayo ni nukuu ya taarifa aliyoiandika Ndimara Tegambwage jana Jumapili, Januari 26, 2013...
Dk. Lwaitama atolewa kwenye ndege, akamatwa na polisi Mwanza

Niliongea na Dk. Azaveli Lwaitama akiwa Mwanza baada ya kuandika maelezo yake kwenye kituo cha polisi cha uwanja wa ndege Mwanza na kuachiwa kwa kilichoitwa "dhamana ya polisi." Anatakiwa kuripoti polisi uwanjani hapo kesho asubuhi kuona iwapo polisi wameamua kumfikisha mahakamani. Nasimulia alivyonisimulia.

Dk. Lwaitama alitoka Dar es Salaam leo asubuhi. Akatua Mwanza. Alikuwa anakwenda Bukoba. Alipanda ndege ya kampuni ileile iliyomtoa Dar es Salaam leo hii - PrecisionAir. Hii ya kwenda Bukoba ilikuwa Na. PW 0492. Alikwenda hadi kwenye kiti chake Na. 2B. Hapa ndipo kuna milango ya dharura kwa pande zote mbili za ndege - kulia na kushoto.

Ndipo akaja mfanyakazi wa ndege. Akamuuliza iwapo anajua Kiingereza. Baada ya mzaha wa kawaida katika kuuliza iwapo 
ni lazima kujua Kiingereza, ndipo mfanyakazi akamwambia kuwa kama hajui lugha hiyo basi ahame kiti na kukaa kwingine kwani kuna maelezo rasmi ambayo yanatolewa kwa "lugha ya anga" - Aviation Language.

Ilikuwa katika kujibizana kwa nini lugha ya anga isiwe lugha ambayo abiria wengi wanaelewa - huku Dk. Lwaitama akisema katika ndege nyingi alizosafiri kote duniani alikokwenda, lugha za anga huwa zile za wasafiri wengi wa eneo husika na lugha nyingine za kimataifa; huku akishauri kuwa maelezo yangekuwa kwa Kiswahili na Kiingereza - ndipo mhudumu alikimbilia mwenzake ambaye naye hakutaka kumsikiliza Lwaitama na wote wawili wakakimbilia kwa chumba cha rubani kushitaki kuwa kuna mtu "anafanya fujo." Tayari Dk. Lwaitama akawa abiria "hatari."

Rubani hakutaka kusikiliza abiria wake anasema nini; hakumuuliza hata mwenzake waliokaa pamoja juu ya fujo alizoripotiwa; alimwambia hawezi kusafiri. Akaita polisi ambao pia hawakuuliza lolote juu ya fujo zake bali walifanya kazi moja ya kumtoa nje mkukuku.

Ni rafiki yake aliyemwita Diallo na mwanaharakati Sungusia ambao anasema aliwapigia simu wampelekee mawakili ili aweze kuandika maelezo yake mbele yao. Mawakili walifika na yeye kuadika maelezo. Mizigo yake imepelekwa Bukoba. Yeye amebaki Mwanza na kompyuta yake ndogo ya mkononi.

Dk. Lwaitama anasema, "Sina mgogoro na kampuni ya PrescisionAir, bali wahudumu ambao hawataki hata kupata maoni ya abiria. Kwanza, walipata bahati ya kuona mtu anahiari maoni moja kwa moja. Pili, kama wanafanya kazi kwenye ndege watakuwa wamesafiri katika ndege za wengine ambako niliyokuwa nayasema ni maneno na vitendo vya kawaida. Sasa fujo ni nini katika hili?

Mwalimu huyo mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anasema, "Hata polisi ni wa kushangaza. Mtu anakwambia huyu kafanya fujo, wewe huulizi ni fujo gani. Unambeba tu mzegamzege. Sidhani kama huu nao ni utendaji bora katika nchi iliyohuru; ambako polisi wanapaswa kuwa na utulivu wa akili na kufanya kazi kwa kufikiri kuliko kwa kuambiwa tu."

Dk. Lwaitana anaamkia kituo cha polisi uwanja wa ndege kesho asubuhi kuambiwa "uamuzi wa polisi."

Haikufahamika iwapo mhudumu wa ndege mswahili, aliyekuwa anaongea Kiswahili, hakuwa na tafsiri ya maneno ya Kiingereza ambayo alitaka kumwambia abiria wake.

ndimara.

No comments:

Post a Comment