Matukio ya raia kutekwa na kuteswa
kinyama kwa kutobolewa baadhi ya viungo vyao vya mwili, kumwagiwa asidi
aina ya tindikali na hata mauaji yanayotokea katika mijumuiko ya kisiasa
ambayo mara nyingi yamekuwa yakidaiwa kuwa na mkono wa Jeshi la Polisi,
huku wahusika wakishindwa kukamatwa na kufikishwa mahakamani, ndiyo
yaliyoibua hisia miongoni mwa jamii inayoielekezea Serikali lawama za
namna hii.
Tayari baadhi ya wanasiasa wenye
ushawishi hapa nchini, viongozi wa dini, wasomi na wanaharakati wa haki
za binadamu, wamekwishakaririwa kwa nyakati tofauti wakieleza kuwa
Serikali ama inapaswa kubeba lawama ama inahusika kwa namna moja au
nyingine na matukio hayo ya kigaidi.
Kauli hizi, zimekuwa zikipata nguvu
kutokana na ugoigoi ambao umekuwa ukionyeshwa na Serikali katika
kushughulikia matukio yenye sura ya kigaidi ambayo sasa yameanza kuota
mizizi licha ya baadhi ya wahanga wa mashambulio ya kigaidi kutoa madai
mazito kwa vyombo vya usalama kwa ujumla au baadhi ya watumishi wa idara
hizo kushiriki kuwatendea unyama huo.
Tukio la hivi karibuni la kumwagiwa
tindikali kwa Padre wa Kanisa Katoliki huko Zanzibar, Anselmo
Mwang'amba, likiwa limetanguliwa na matukio mengine kadhaa ya aina hiyo
yaliyotokea katika kipindi kifupi nyuma kwa raia wa kigeni, wananchi wa
kawaida na viongozi wa dini ya Kiislamu, ndilo linaloonekana kuizamisha
Serikali kwenye tope hili, baada ya baadhi ya mapadre kuinyooshea kidole
moja kwa moja Serikali kuwa chanzo cha kutekelezwa kwa uovu huo.
Padre Mwang'amba alimwagiwa tindikali
na watu ambao hawajafahamika, wakati akiwa nje ya mgahawa wa Internet,
huko Zanzibar, lakini baadhi ya mapadre wenzake waliomsindikiza
Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu zaidi,
walilieleza kuwa wanaamini waliotekeleza uhalifu huo ni watu wanaotaka
sauti za Wazanzibari za kuukataa muundo wa sasa wa Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar zisikilizwe.
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Jimbo
Katoliki la Zanzibar, Padre Arbogast Mushi, wiki iliyopita alisema kuwa,
sauti za wananchi wa Zanzibar zinasikika zikiupinga muungano wa sasa wa
Tanganyika na Zanzibar.
Alisema, matukio ya kinyama
yanayofanywa sasa yakiwalenga viongozi wa dini na watu wengine katika
jamii, yanalenga kushinikiza visiwa hivyo kuachiwa huru.
Padre Mushi alisema jamii kubwa ya
watu wa Zanzibar ni waumini wa dini ya Kiislamu, hivyo lipo kundi dogo
la watu ambalo limeamua kushinikiza sauti za Wazanzibari zisikilizwe kwa
kutumia njia hizo chafu, kulazimisha mamlaka kuchukua hatua na pia
kuwatisha wasio waumini wa dini hiyo kuamini kuwa Zanzibar siyo sehemu
salama ya kuishi kwa mtu ambaye siyo Muislamu.
Kauli hiyo ya Padre Mushi inafuatiwa
na ile iliyotolewa jana na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wakristu Tanzania
(CCT), Askofu Peter Kitula, katika mahojiano yake kupitia simu yake ya
kiganjani akimtaka Rais Jakaya Kikwete kuchukua hatua za haraka za
kuufumua uongozi wa Jeshi la Polisi, kwa kuwaondoa watendaji wake wa
sasa na kuweka wapya wenye uwezo wa kulinda uhai wa Watanzania.
Askofu Kitula ambaye alikuwa akieleza
msimamo wa jumuiya anayoiongoza kuhusu kushamiri kwa vitendo vya
uvunjifu wa amani nchini, alisema Serikali imeruhusu wageni kuingia
nchini kiholela na kusababisha Watanzania kuiga mwenendo wa maisha yao
hususan wanaotoka katika nchi zenye machafuko.
"Watu wengine kweli ni magaidi,
wanakuja kwa maslahi yao, wanawatumia Watanzania kutenda mambo ya
kihalifu. Kwa hali hii Serikali inatakiwa kuwachukulia hatua haraka
watuhumiwa wa matukio haya.
"Kitendo cha kuendelea kukaa kimya,
hakileti picha nzuri kwa jamii, Serikali inaonyesha imeshindwa
kuwakamata, inajipaka matope ya damu ya wananchi wake," alisema.
Kiongozi mwingine wa dini
aliyezungumzia mwenendo huo wa mambo, ni Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Alhad Mussa Salum, ambaye aliionya Serikali kuhusu tume
inazounda kuchunguza matukio ya kigaidi dhidi ya raia.
Shekh Salum alisema tume zote za
uchunguzi zinazoundwa kuchunguza matukio ya kihalifu yenye sura ya
kigaidi, hazitoi majibu ya uchunguzi huku zikiwa zimetumia gharama kubwa
ambayo ni kodi ya wananchi.
"Wananchi wanapata wasiwasi kwamba,
kwanini tume hizi hazileti mrejesho, Serikali inatakiwa kuhakikisha
mambo haya yanawekwa sawa ili kuondoa mawazo mabaya kuwa labda matukio
haya yanatokana na mgongano wa kiimani," alisema.
Kauli ya Sheikh Salum kuhusu wasiwasi
wa utendaji wa tume zinazoundwa na Serikali kuchunguza matukio
mbalimbali ya kigaidi dhidi ya raia ambayo pia imezungumzwa na watu
mbalimbali waliohojiwa na MTANZANIA Jumatano, inaibua upya kumbukumbu ya
tume kadhaa zilizopata kuundwa kuchunguza vitendo vya uhalifu dhidi ya
raia ambazo hadi sasa hazijatoa majibu ya uchunguzi wake.
Miongoni mwa tume hizo ni ile
iliyoundwa kuchunguza tukio la kuvamiwa, kujeruhiwa na kupigwa vibaya
kwa Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania na Mhariri Mtendaji Mkuu
wa Kampuni ya New Habari (2006) Ltd, Absalom Kibanda, mwezi Machi mwaka
huu.
Kibanda alitendewa vitendo vyenye sura
ya kigaidi, huku wakati akiwa na mgogoro na Serikali kutokana na
mitizamo na misimamo yake ya kazi ya uandishi wa habari.
Siku chache baada ya kuteswa, iliundwa
tume iliyokuwa na makachero wenye ujuzi na uzoefu wa kazi ya kikachero
kuchunguza tukio hilo, lakini hadi sasa ikiwa ni zaidi ya miezi sita
tangu alipopatwa na mkasa huo, taarifa ya tume iliyoundwa haijawahi
kutoka na kumekuwa na tetesi nyingi kuwa huenda shambulio hilo
lilitekelezwa na wanataaluma ya utesaji ambao aghalabu wanapatikana
katika vyombo vya dola.
Tume nyingine ambayo inachukua
mwelekeo unaofanana na iliyoundwa katika sakata la Kibanda, ni ile
iliyopewa jukumu la kuchunguza sakata ka kutekwa na kuteswa kinyama kwa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk. Steven Ulimboka.
Dk. Ulimboka aliteswa kinyama na kabla
ya kutupwa kwenye msitu wa Mabwepande ulio nje kidogo ya Jiji la Dar es
Salaam, ambako aliokotwa baadaye na wasamaria wema waliomfikisha
Hospitali ya Muhimbili kwa matibabu.
Saa chache baada ya kuokotwa, alieleza
kuwatambua waliomteka na kumtesa na alimtaja mmoja wa wanausalama
kuhusika na tukio lake, lakini tume iliyoundwa kuchunguza ukweli wa
tukio lake ambayo pia ilikuwa na makachero wenye ujuzi na uzoefu wa kazi
ya ukachero, hadi sasa ikiwa ni takribani zaidi ya mwaka mmoja,
haijawahi kutoa majibu wala tamko lolote la uchunguzi wake.
Mkurugenzi wa Kituo cha Haki za
Binadamu (LHRC), Hellen Kijo Bisimba, ambaye alihusika kwa karibu
kumsaidia Dk. Ulimboka, baada ya kuteswa, kiuhalisi matukio yote ya
kigaidi yanayotokea sasa nchini yanaonekana kuwa na mkono wa Serikali na
ndio maana hakuna hatua stahiki inazochukua kukabiliana nayo.
Bisimba alisema yapo baadhi ya matukio
ambayo yaliigusa Serikali moja kwa moja na kuchukuliwa hatua za haraka
kwa watuhumiwa kukamatwa, lakini mengine imekuwa ikizungusha.
"Matukio yasiyoigusa Serikali
hawahangaiki nayo wanabaki kutubabaisha tu, kwa mfano lile la mauaji ya
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, pamoja na lile la
askari mmoja wa usalama barabarani aliyegongwa, tuliona mara moja
watuhumiwa walikamatwa ndani ya muda mfupi na kuchukuliwa hatua,"
alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo,
Serikali inatakiwa kuweka pembeni unafiki na kutekeleza wajibu wake ili
kujinasua na harufu ya damu ya watu wake inayotoa sasa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es
Salaam, Dk. Azaveli Lwaitama, ambaye pia alizungumza kuhusu mwenendo wa
sasa wa usalama wa raia, yeye alilitaka Jeshi la Polisi likatae kuwekwa
mfukoni na CCM pamoja na wanasiasa na badala yake lifanye kazi yake kwa
kuzingatia taratibu na maadili ya kazi zake.
Alisema asilimia kubwa ya matukio ya kigaidi yanayoendelea kutokea yanaigusa Serikali na Jeshi la Polisi.
"Kila tukio utasikia ni ugaidi, udini,
Muungano, haya ni mambo ambayo chanzo chake ni siasa, tuache siasa
tufanye kazi, tukiendelea hivi tutafikia pabaya," alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama
cha Wananchi (CUF), Ibrahim Lipumba, alilitupia lawama Jeshi la Polisi
kwa kushindwa kuwakamata wahusika wanaomwagia raia tindikali.
Lipumba alisema kuwa uwepo wa matukio
ya kigaidi nchini ni matokeo ya kuwa na Jeshi la Polisi lililotawaliwa
na tatizo la ukosefu wa weledi na intelijensia ya uhakika, ambayo
ingeweza kuyamaliza matatizo yote ya kinyama yanayotokea sasa.
Alisema Zanzibar ni nchi ndogo, ambayo
haiwezi kulifanya Jeshi la Polisi kushindwa kuwakamata wahusika
wanaomwagia watu tindikali, lakini kwa sababu jeshi hilo limetawaliwa na
siasa, limekuwa likiishia kutoa matamko yasiyo na tija kwa Taifa.
Mwanasiasa mwingine aliyezungumza na
kutoa maoni yake kuhusu usalama wa raia nchini iwapo unaridhisha, ni
aliyewahi kuwa mgombea urais wa Chama cha NCCR-Mageuzi, ambaye kwa sasa
ni Mwenyekiti wa Chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe
ambaye alisema Serikali haiwezi kukwepa lawama za matukio ya kigaidi,
kwa sababu kwa kiasi kikubwa wasaidizi wa rais wameshindwa kumsaidia
kupambana nayo.
"Rais Kikwete amejitahidi kutaka
kutekeleza mikakati yake, lakini baadhi ya viongozi aliowateua wamekuwa
hawana msaada kwake na ndio wao wanakuwa chanzo cha vurugu hizi,
kutokana na kushindwa kwao kuwa na mikakati imara ya kupunguza tatizo la
ajira.
"Ugumu wa maisha unachangia kuibuka
kwa matukio ya kikatili kama haya, ni jambo rahisi kumnunua mtu fukara
kwa vijisenti kidogo ili afanye unyama, lakini haiwezekani kufanya hivyo
kwa mtu mwenye shughuli ya kumuingizia kipato.
Alipoulizwa Msemaji wa Jeshi la
Polisi, Advera Senso, kuhusu mtizamo huo ilionao jamii kwa sasa kuhusu
taswira ya Serikali katika kushughulikia vitendo vya kigaidi, alijibu
kwa ufupi kuwa hawezi kutoa jibu la jambo hilo na baadaye aliliomba
gazeti hili kutafuta muda wa kufanya naye mahojiano ofisini kwake.
"Nakuomba uje ofisini, hili suala ni
pana sana, njoo tufanye mazungumzo ya kina, naomba uje ofisini
tulizungumze kwa kina," alisema Senzo.
Chanzo: Mtanzania