Ni baada ya miili saba ya wanajeshi waliouawa Darfur kuwasili Dar
Kuagwa kesho...kila mpiganaji aliyeuawa atafidiwa sh. milioni 113
Kuagwa kesho...kila mpiganaji aliyeuawa atafidiwa sh. milioni 113
Askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania wakiwa
wamebeba moja ya majeneza saba yaliyobeba miili ya wanajeshi waliokuwa
katika kikosi cha Umoja wa
Mataifa cha walinda amani wa Darfur nchini
Sudan.
Vilio na mayowe jana vilitawala Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Mwalimu J.K Nyerere jijini, Dar es Salaam, wakati miili
ya askari saba wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) ilipowasili kutoka
Dafur nchini Sudan.
Askari hao waliuawa Jumamosi iliyopita kwenye shambulizi la kushtukiza, huku wengine kujeruhiwa.
Ndugu wa marehemu wakiwemo watoto, wake
zao na marafiki walikuwa wakilia wakati wote tangu miili hiyo
ilipowasili uwanjani hapo na kushukia Terminal 1-Air wing (kikosi cha
anga).
Baadhi ya jamaa za marehemu walishindwa kuzungumza , wengine wakishikiliwa kuwazuia wasianguke kutokana na huzuni ya msiba huo.
Ndege maalum ya Umoja wa Mataifa (UN) yenye namba B 737- 400 COMBI, ilileta miili hiyo na kutua uwanjani hapo saa 10:45 jioni.
Miili hiyo iliondolewa na kuingizwa katika
magari saba ya JWTZ kila mmoja ukisafirishwa peke yake kwenye msafara
ulioongozwa na pikipiki za jeshi na kupelekwa Hospitali ya Jeshi
Lugalo.
Makamu wa Rais Dk. Mohamed Gharib Bilal,
aliwaongoza viongozi wa serikali akiwamo Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi,
Jenerali Davis Mwamunyange, pamoja na mamia ya wananchi waliofika
uwanjani kuwapokea marehemu hao.
Naye Kaimu Mkurugenzi wa Habari wa JWTZ,
Meja Joseph Masanja, alisema marehemu wataagwa kesho saa 2:30 asubuhi
katika viwanja vya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Upanga
jijini.
Alisema miili hiyo itaagwa kwa heshima zote za kijeshi na baadaye kusafirishwa kwa ajili ya mazishi.
Akizungumza uwanjani hapo, msemaji wa
familia ya Sajenti Shaibu Othumani, alisema wamepata pigo kubwa kwa kuwa
ndugu yao alikuwa tegemeo katika familia hiyo.
Shemeji wa marehemu Othuman aliyejitaja
kwa jina la Rehema akizungumza huku akiwa analia alisema wamepatwa na
majonzi na kwamba ni vigumu kumsahau mtu waliyetoka naye mbali.
Wanajeshi hao ni Sajenti Othuman ,
makoplo Oswalid Chacha, Mohamed Juma na Mohamed Chukilizo. Wengine ni
maprivate Rodney Ndunguru , Peter Werema na Fortunatus Msoffe.
FIDIA KWA MAREHEMU
Kila mpiganaji aliyeuawa atafidiwa Dola
za Marekani 70,000 ( karibu Sh. milioni 113) kwa mujibu wa viwango vya
Umoja wa Mataifa (UN).
Fedha hizo zimetajwa na vyombo vya habari
vya kigeni kuwa ni kiwango kinachotolewa na UN kwa askari anayeuawa
akiwa kwenye operesheni za kulinda amani zinazosimamiwa na chombo hicho.
Wapiganaji saba kati ya 14 wa JWTZ
walioko Dafur kwenye kikosi cha kulinda amani kinachoundwa na UN
pamoja na Umoja wa Afrika (Unamid), Jumamosi iliyopita waliuawa baada ya
kushambuliwa kwenye tukio la kushtukiza.
Chini ya utaratibu wa UN wa fidia, kila
mpiganaji aliyepoteza maisha atafidiwa Dola 70,000 kwa mujibu wa
taarifa za Radio Sauti ya Ujerumani (DW) Idhaa ya Kiswahili,
zilizotangazwa jana asubuhi.
DW ilifanya mahojiano na Kaimu Msemaji wa
Kurugenzi ya Mawasiliano ya JW, Meja Joseph Masanja na kumhoji kuhusu
fidia hiyo kutolewa kwa jamaa waliopoteza ndugu zao .
Akijibu Kaimu Msemaji wa JW alisisitiza
kuwa fidia ya marehemu hao itakuwepo lakini hakupinga kiwango cha (UN)
wala kukubali badala yake alisema kinachofanyika kwa wakati huu ni
kuwaleta marehemu hao nchini na kuwafikisha sehemu ambazo jamaa zao
wamezitayarisha kwa ajili ya kuwazika.
Kama familia hizo zitafidiwa kiasi hicho,
kila aliyepoteza jamaa yake atapokea zaidi ya Sh milioni 100 bila
kuhusisha fidia kwa taifa. (Dola ni karibu Sh 1,620).
Katika mahojiano hayo, Kaimu Msemaji wa
JWTZ aliulizwa iwapo serikali ina mpango wa kuwafidia askari hao, hata
hivyo alikwepa kujibu swali hilo na kuzungumzia zaidi juu ya kuwapokea
na kuwazika.
CHANZO:
NIPASHE JUMAPILI
No comments:
Post a Comment