Bila shaka kila mwananchi anayeitakia
mema nchi yetu amevutiwa na habari zilizochapishwa katika gazeti hili
jana kwamba vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi
(Ukawa), vimeamua kushirikiana katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa
kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi ya urais, ubunge na udiwani.
Viongozi wakuu wa vyama hivyo tayari
wamekubaliana kuanza mchakato huo na wameandika mapendekezo na
kuyapeleka katika sekretarieti za vyama vyao kwa ajili ya kufanyiwa
uchambuzi.
Sisi tunaona kitendo hicho cha vyama
vinavyounda Ukawa kuwa ni hatua muhimu ya kuongeza nguvu ili kuongeza
ushindani ambao ni muhimu katika mustakabali wa nchi yetu kisiasa na
hivyo kusaidia nyanja nyingine za kiuchumi na kijamii.
Tangu kuruhusiwa tena kwa siasa huru
karibu miaka 22 sasa, bado nchi haijashuhudia ushindani wa kweli
unaoweza kuwafanya watawala kuwajibika kwa wananchi kutokana na kuona
hatari ya kuondolewa madarakani na vyama pinzani.
Hii imetokana na vyama shindani katika
siasa kukumbwa na mifarakano ya kisiasa ambayo imekuwa ikiwagawa na
hivyo kuingia kwenye chaguzi vikiwa dhaifu na hivyo kushindwa vibaya na
chama tawala na matokeo yake yamekuwa ni wananchi wengi kukata tamaa na
hivyo kusababisha idadi ya wanaoshiriki kupiga kura kupungua mwaka hadi
mwaka kutokana na kutoona faida ya siasa za ushindani.
Pengine hiyo ndiyo sababu iliyofanya
wananchi wapendekeze kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba kwamba vyama
viruhusiwe kuunganisha nguvu wakati wa chaguzi kwa kuwa wameona bila ya
nguvu ya vyama shindani, watawala wawataendelea kuongoza kwa mazoea na
matokeo yake ni wananchi kuendelea na umaskini wao na kuona uhuru wa
vyama vya kisiasa hausaidii kuwa kuboresha maisha yao.
Si nia yetu kuona chama tawala
kikiondolewa madarakani na vyama shindani, lakini tunachotaka kuona na
ushindani wa dhati, makini na wa kweli ambao, kwa taifa lolote lile, ni
afya kwa ustawi wa wa taifa kwa kuwa huongeza uwajibikaji kwa watawala.
Hakuna ubishi kwamba upinzani wenye
nguvu huisukuma serikali ichape kazi na kuwatumikia wananchi kwa
kutambua kwamba ikiboronga itaondolewa madarakani na serikali kivuli
ambayo ni vyama vya upinzani.
Vyama legelege vya upinzani huogopa
kivuli cha serikali na kufifisha maendeleo na kuzima matumaini ya
wananchi wanaotaka kuona uwajibikaji serikalini, kwani huwa chachu ya
kuendeleza tawala za kiimla zisizothamini demokrasia na zisizowajibika
kwa wananchi.
Ndiyo maana tunawapongeza viongozi wa
Ukawa kwa kuona umuhimu wa kuunganisha nguvu na kuwa wamoja ili kuweka
ushindani wa kweli katika mazingira ya kisiasa tuliyomo.
Tunachoweza kuwashauri viongozi wa
Ukawa ni kuwa makini na kuondoa tofauti zinazowatenganisha. Ukawa
isitarajie kwamba kila kitu kitakuwa mteremko, kwani bado sheria
kandamizi ambazo zimekuwa zikikwaza shughuli za upinzani bado
hazijafutwa.
Ni matarajio yetu kwamba serikali na
chama tawala kitachukulia hatua hiyo ya Ukawa kuwa changamoto ya
kuongeza ufanisi katika kuwatumikia wananchi na si kuanza kujenga chuki
na kutafuta mbinu za kuikwamisha
Serikali haina budi kuhakikisha kuwa
vyama vyote vinapewa nafasi sawa ya ushindani na kujengewa mazingira ya
kukua ili kukifanya chama chochote kinachopewa madaraka kiwajibike kwa
wananchi na kuwaletea maendeleo.(E.L)