Friday, March 7, 2014

Safari ya kupata Katiba Mpya giza totoro mbele

Mwenyekiti wa muda Bunge la katiba,Pandu Kificho.
Bunge Maalumu la Katiba lililoanza Februari 18, mwaka huu, limeendelea kuonyesha dalili za kuwa na hatima mbaya katika safari yake, inayokusudia kujadili na hatimaye kupitisha Rasimu ya Katiba ya Mwaka 2013, iliyotolewa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba.
Hiyo ni kutokana na hofu itokanayo na kuwapo kwa kila dalili kwamba Bunge hilo linaweza lisifikie lengo kuu ambalo ni kuipitisha rasimu hiyo baada ya kuijadili.

Rasimu hiyo imepangwa kuwasilishwa na Mwenyekiti wa Tume hiyo, Jaji Joseph Warioba, baada ya Rais Jakaya Kikwete, kulizindua Bunge hilo, pamoja na makatibu, mwenyekiti na wajumbe wake kuapishwa.

Kinyume cha mwongozo na wosia uliowahi kutolewa na Rais Kikwete wakati yeye na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Shein, wakikabidhiwa rasimu hiyo na Tume ya Mabadiliko ya Katiba, hivi sasa wajumbe wa Bunge hilo wamegawanyika katika makundi makubwa mawili hasimu.

Kundi la kwanza, linaongozwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia wajumbe, ambao ni wanachama wake waliomo kwenye Bunge hilo.

La pili, linaundwa na wajumbe kutoka vyama vya upinzani, baadhi ya wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Baraza la Wawakilishi la Zanzibar, baadhi ya mashirika yasiyokuwa ya kiserikali na taasisi za kidini.

Mvutano baina ya makundi hayo mawili, umedhihirika wakati wa mjadala wa Rasimu ya Kanuni za Bunge Maalumu za Mwaka 2014.

Mjadala huo ulifanyika kupitia semina iliyotolewa kwa wajumbe hao bungeni, Jumatano na Alhamisi, wiki iliyopita.

Pamoja na mambo mengine, mgawanyiko mkubwa baina ya wajumbe hao unatokana na ibara ya 37 kifungu cha (3) na cha (4) vya rasimu ya kanuni hizo.

Vifungu hivyo vinapendekeza utaratibu utakaotumiwa na Bunge Maalumu kupata uamuzi katika vikao vyake.

Katika utaratibu huo, vifungu hivyo vinapendekeza kuwa baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu kutoa swali la kulihoji Bunge, itapigwa kura ya siri, ambayo itaitwa “kura ya mwisho.”

Vifungu hivyo vinaeleza: “Kwa madhumuni ya Kanuni hii, utaratibu utakaotumika kupata uamuzi baada ya Mwenyekiti wa Bunge Maalumu kutoa swali la kulihoji Bunge Maalumu utakuwa ni wa kura ya siri.”

“Bila kuathiri masharti ya Sheria na Kanuni hizi, wakati wa kupata uamuzi Bunge Maalumu kuhusu kupitisha Rasimu ya Katiba, Bunge Maalumu litapiga kura ya siri, ambayo kwa madhumuni ya Kanuni hii, itaitwa “kura ya mwisho.”

Kundi la kwanza la wajumbe, wengi wakiwa ni wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi la Zanzibar kutoka CCM, baadhi ya viongozi wa dini na makundi ya kijamii, wanataka utaratibu utakaotumiwa na Bunge Maalumu kupata uamuzi uwe wa kura za wazi.

Kundi la pili, linaloongozwa na vigogo wa vyama vya upinzani, wajumbe wengi kutoka makundi ya kijamii na baadhi ya viongozi wa dini na wabunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wakiwamo wachache wa CCM, wanataka utaratibu utakaotumiwa uwe wa kura za siri.

Hoja ni nyingi zinazotolewa na kundi la kwanza kushikilia msimamo wake wa kura ya wazi.

Lakini kubwa ni kwamba, wanadai kuwa utaratibu wa kura ya wazi utawawezesha wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba kuwaonyesha watu wanaowawakilisha nini wameamua bungeni yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba.

Kundi hilo linadai kuwa utaratibu wa kura ya siri katika kuamua kuhusu kitu kama katiba ni wa woga na una mbaya kutaka kuficha nia ovu ya rushwa.

Kundi la pili, nalo pia lina hoja nyingi linazoziona kuwa ni halali kung’ang’ania msimamo wake wa kutaka utaratibu wa kupata uamuzi kwa kupiga kura ya siri.

Kubwa ni kwamba, linadai kuwa utaratibu wa kura ya siri ni wa kidemokrasia na pia unazingatia uhuru wa mtu, haki za binadamu na unalinda usalama wa mtu dhidi ya vitisho, ambavyo anaweza kuvipata kutoka kwa viongozi wake iwapo watatofautiana katika misimamo na maamuzi.

Vilevile, wanadai kuwa ni utaratibu unaotumika pia katika kuchagua viongozi wa kisiasa, kama vile mwenyekiti wa serikali ya mtaa, diwani, mbunge na hata rais.
Mbali na kauli ya kamati ya kanuni iliyoongozwa na Profesa Costa Mahalu, kwamba hoja za kila upande zina misingi wa kidemokrasia, hali bado ni tete baina ya makundi hayo mawili ya wajumbe wa Bunge hilo. 
Pamoja na mambo mengine, kubwa ni kwamba, hali hiyo inaonekana kuwa inatokana na kila upande kushikilia msimamo wake na kutokuwa tayari kuridhia msimamo wa mwingine.

Hapo ndipo pia wengi wanaposhindwa kuelewa mantiki ya ushauri uliotolewa na kamati ya kanuni kwamba, utaratibu utakaotumiwa na Bunge Maalumu kufanya uamuzi, uamuliwe na wajumbe wenyewe!

Hawa tayari wana ukinzani mkubwa huku kila siku wakiingia bungeni, kazi ni kubishana na kuvutana! Hilo wanalorejeshewa waliamue ndilo la kuja kuwaongoza baadaye, linawagawa.

Je, watawezaje kulitatua wenyewe? Na walitatue kwa utaratibu gani, ambao utaridhiwa na kila kundi?

Ni dhahiri kuwa kila anayefuatilia mvutano huo, ana wasiwasi mkubwa juu ya uwezekano wa hali hiyo kuzifanya pande mbili hizo kutofikia suluhu.

Tayari wabunge wa CCM wameshakutana mara mbili kupeana mikakati na kujipanga namna ya kushiriki vikao vya Bunge hilo.

Upande mwingine, wajumbe wengine wa Bunge hilo, wakiongozwa na baadhi ya vigogo wa vyama vya upinzani nchini, wameunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Mjumbe wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba, anasema lengo la kuunda umoja huo ni kukabiliana na njama zozote za rasimu ya katiba kuchakachuliwa katika Bunge hilo.

Yote tisa. Lakini kumi, sababu kubwa ya mvutano huo ni muundo wa Muungano. Kundi moja linataka uwe wa serikali tatu, kama inavyopendekezwa kwenye Rasimu ya Katiba na mwingine unataka uwe wa serikali mbili.

Pengine suala hilo pamoja na mambo mengine yaliyomo kwenye Rasimu ya Katiba ndiyo yaliyomfanya Rais Kikwete kushtuka na siku aliyokabidhiwa rasmi ya Pili aliwataka wajumbe kujadiliana na kukubaliana bungeni vingine watashindwa kupata Katiba Mpya inayopendekezwa.

Itakumbukwa namna alivyowahi kuwasihi wajumbe watakaojaliwa kuingia kwenye Bunge hilo kutumia busara kikamilifu wakati wa kuijadili Rasimu ya Katiba ili matunda yanayotarajiwa na wananchi yapatikane kwa ajili ya Watanzania wote na siyo watu au kikundi fulani cha watu au taasisi fulani.

Rais Kikwete alisema dhamana ya Tanzania na Watanzania ipo mikononi mwa wajumbe hao, hivyo akawasihi wawe makini kwa kutambua nini Watanzania wanahitaji, badala ya kuweka mbele maslahi yao, itikadi, mapenzi na ushabiki wa kimakundi.

Kwa uchache, alisema iwapo watafanya mchezo, mbali na kukosa katiba nzuri, watakosa katiba mpya kabisa.

Kwa mvutano uliopo baina makundi hayo mawili, ni wazi kuwa sasa naanza kumuelewa Rais Kikwete. Kwamba, aliona mbali na dalili za kutofikiwa kwa suluhu katika Bunge hilo zinaanza kuonekana.

Kinachoonekana ni wajumbe kutunishiana misuli ya kiitikadi, huku wakisahau kuwa wanachojadili ni hatima ya nchi.

Hawataki kabisa kuweka vyama vyao kisogoni na kuweka nchi kwenye paji la uso wakati wa mijadala yao.

Iwapo hali hii itaendelea na wajumbe hawatotumia busara, ni wazi kuwa hata wakiongezewa mwaka, kamwe suluhu haiwezi kupatikana.

Na iwapo suluhu itakosekana, wajue kuwa wananchi watachoka, wataandamana kumuomba Rais asilizindue Bunge hilo.

Kwani wananchi wana mahitaji mengi. Iweje yatumike mabilioni ya shilingi kwa Bunge ambalo halina tija?

Maana kuna hatari mvutano unaoendelea wa rasimu ya kanuni za Bunge Maalumu ‘kutafuna’ hizo siku 70 za Bunge hilo huku zikiendelea kutetketeza mabilioni ya shilingi za walipakodi, huku suluhu ikikosekana.

Kwa sababu wataendelea kubishana tu kila siku, huku wakiwa hawana kanuni zinazowaongoza wala kuapishwa.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment