Katika maisha ya kawaida, binadamu ana msimamo wake na hata uamuzi asiopenda ubadilike.
Katika
medani ya siasa nchini msimamo wa Chama Cha Mapinduzi ( CCM) kuhusu
Muungano na muundo unafahamika. Ni muundo wa kutaka Serikali mbili ambao
chama hicho unakipigania kwa udi na uvumba.(Hudugu Ng'amilo)
Hata
hivyo, msimamo huo ni kinyume na mapendekezo au matakwa ya wengi kama
ilivyoainishwa kwenye Rasimu ya Pili ya Katiba iliyoandaliwa na Tume ya
Mabadiliko ya Katiba.
Tume hiyo
iliyokuwa chini ya Jaji Joseph Warioba ilikusanya maoni ya wananchi na
ilipendekeza muundo wa Muungano wa Serikali tatu.
Hivi
karibuni akifungua Bunge Maalumu la Katiba, Rais Jakaya Kikwete akaunga
mkono msimamo wa chama chake, jambo lililoibua mjadala unaoendelea hadi
sasa.
Hoja ya Serikali mbili
Kwanini
CCM wanataka Serikali mbili na siyo tatu au moja kama ilivyo maoni ya
wananchi walio wengi kwa mujibu wa maelezo ya Tume ya Warioba? Makala
haya yanachambua hoja hiyo.
Profesa
Bakar Mohammed ni Mhadhiri Mwandamizi na Mkuu wa Idara ya Siasa na
Utawala ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, anayesema msimamo wa CCM wa
kudai Serikali mbili unatokana na hofu ya uhafidhina wa kuogopa
mabadiliko.
Anasema
viongozi wengi wa CCM wanasumbuliwa na hofu na woga wa mabadiliko na
kwamba wanakuwa wagumu kuyakubali yanapotaka kutokea.
"Kama mtu
unaangalia madaraka zaidi, lazima kunakuwa na woga, na hii ni hulka ya
binadamu kuwa na woga wa kuacha kile ulichokizoea... Lakini ukiangalia
masilahi ya nchi na kuacha yale yanayokusukuma kusingekuwa na wasiwasi
huu unaoonekana sasa," anasema.
Anasema
CCM inachofanya ni kuhakikisha haking'oki madarakani, huku viongozi wake
wakiamini kuwa wana sifa za kuongoza na siyo wengineo.
Profesa
Bakari anailinganisha hofu ya sasa ya CCM na ile waliyokuwa nayo
viongozi wa chama hicho miaka ya 1990 zilipoanza vuguvugu za mabadiliko
ya siasa za vyama vingi. Anasema CCM kiliendesha propaganda kuwa mfumo
wa vyama vingi haukuwa na tija na ungeleta vita.0
inShare
Hofu hiyo anasema ndiyo inayokifanya chama hicho kikongwe kuhofia kung'olewa madarakani.
"Woga huo
bado upo, wanaogopa pengine mfumo ukiwa wa Serikali tatu uwezekano wa
wao kubaki madarakani utakuwa mdogo," anafafanua.
Anaongeza kusema kuwa hofu ya CCM siyo kwa ajili ya masilahi ya nchi, badala yake inaonekana chama kinaangalia masilahi yake.
Ingekuwa vyema anasema kwa CCM kueleza madhara yanayoweza kulikumba taifa ikiwa muundo wa Serikali tatu utapita.
"Wanatoa
hoja kuwa mfumo wa Serikali tatu unaweza kusambaratisha nchi, lakini
hakuna uhakika kama mfumo huu uliopo nchi hauwezi kusambaratika,"
anasema.
Hofu ya kuyumba na kuanguka
Mhadhiri
mwingine wa chuo hicho, Dk. Benson Bana anasema siri ya CCM
kung'ang'ania Serikali mbili inatokana na hofu ya kuyumba na kuanguka.
Anasema
CCM kimekuwa madarakani na mfumo huo kwa miaka 50 na kwamba hofu yao ni
kuwa ukiondoa Serikali mbili kinaweza kuyumba na kuachia madaraka.
Anasema misingi ya wanasiasa ni madaraka, na kwamba ukishayapata, huwezi kuyaachia kirahisi.
"Misingi
ya wanasiasa ni madaraka... Kuyalinda, kuyahifadhi na kuyatumia madaraka
yale kwa namna yoyote...Huwezi kuyaachia madaraka kirahisi. Utafanya
ujanja, utatumia mbinu chafu ili tu kuhakikisha unabaki madarakani, na
hiki ndicho wanachofanya CCM," anasema.
Dk. Bana anasema CCM kingeeleweka na kingekuwa na mwonekano mzuri zaidi endapo wangepigania kuwapo kwa Serikali moja.
"Wangekuwa
wanataka muungano imara, endelevu na uliokomaa wangeelekeza katika
Serikali moja...Lakini hawataki kwa sababu wanajua moja inaweza
ikawanyima uongozi," anasema.Dk. Bana anasema ni vyema wananchi
wakaelimishwa huu muungano una faida gani na wanafunzi shuleni katika
elimu ya uraia waelezwe faida zake.
"Ingekuwa
wazi tungejua nani anafaidika na nini, mikopo misaada, nani anachangia
nini...Je zile sababu za waasisi za kuungana bado zipo sasa miaka 50 ya
Muungano, ule woga kuwa Zanzibar itamezwa bado upo leo?" Anahoji.
Anaongeza
kuwa ni vyema kwa watawala kutazama mazingira ya sasa ya siasa zetu kwa
kile anachoeleza kuwa hata Katiba ikipita ikakubali kuwapo wa Serikali
mbili, bado wananchi watahoji mantiki ya muundo huo.
Msomi
mwingine wa siasa, Dk. Alexander Makuliko anasema hofu ya CCM ni kuwa
ndio iliyouasisi Muungano wa Serikali mbili, hivyo isingependa hali hiyo
ibadilike.
Anaendelea
kusema kuwa CCM imezoea mfumo huu na kuwa ikiukosa itaathirika, kwakuwa
ni sera yake na imekuwa ikiitekeleza, lakini msimamo wa wananchi ndiyo
kitu cha msingi kuzingatiwa. Hoja zijengwe na zisikilizwe, ubabe
hautakiwi, busara inahitajika zaidi.
Anasema
pamoja na suala la Serikali mbili kuwa ni pimajoto ya uhai wa CCM, hata
hivyo hoja zinazotolewa katika kutetea msimamo wao ni nzuri tu na
zinazoeleweka vyema.
"Sioni
kama wanang'ang'ania, lakini ukweli ni kuwa kila chama kina sera yake,
na CCM kimeweka sera yake katika suala la Muungano wao wanasema ni
Serikali mbili, na siyo tatu...kwamba tatu zitaongeza gharama na
mengineyo, ni sababu za msingi kabisa," anasema.
Anaongeza
kuwa hoja zinazotolewa na chama tawala ni kubwa na siyo za kupuuzwa,
lakini vilevile kero zinazotajwa kuhusu mfumo wa Muungano uliopo nazo
zipo na zinaweza kutatuliwa katika mfumo uliopo.
"Unajua
hivi vyama kila kimoja kinataka kuvutia kwake, hata bila rasimu ya
Warioba...Ninashauri walete hoja, kisha watu wazipime hizo hoja, kwanini
serikali mbili, na wale wa tatu tayari wameleta hoja na ushahidi, watu
waachwe wapime," anasema na kuongeza:
''Jambo
la msingi kuzingatiwa ni kuwa mawazo ya wananchi wengi yataonekana
wakati wa kura za maoni. Angalizo ni kuhakikisha kuwa kura hiyo isije
ikachakachuliwa.''
CHANZO MWANANCHI
No comments:
Post a Comment