Wiki ya
Machi 18 - 22, 2014, mwenyekiti Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji
Joseph Warioba aliwasilisha Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania kwenye Bunge la Katiba.
Wiki hiyo
iliishia siku ya Ijumaa ambayo Rais wa Jamhuri ya Muungano, Jakaya
Mrisho Kikwete alitoa hotuba kwa Bunge hilo Maalumu.
Hotuba
zote zilipokelewa kwa hisia tofauti kulingana na msimamo wa kila mtu
kuhusu hoja inayoonekana ni kubwa kuliko zote katika Mchakato wa
Kuandika Katiba Mpya, hususan suala la Muundo wa Muungano.(Hudugu Ng'amilo)
Wale
wanaoshabikia muundo wa serikali tatu, walifurahishwa mno na hotuba ya
Jaji Warioba na wanaoshabikia muundo wa serikali mbili, walifurahishwa
mno na hotuba ya Rais Kikwete. Mimi Sikufurahishwa na hotuba zote mbili
kwa sababu zifuatazo;
Hotuba hazikunifurahisha
Moja,
hotuba zote mbili zilichukua muda mrefu zaidi kuelezea sura moja tu ya
Rasimu ya Katiba nayo ni sura ya Sita inayohusu muundo wa Jamhuri ya
Muungano kana kwamba Katiba hii inahusu suala hilo pekee.
Ni
dhahiri kwamba suala hili ni kubwa na muhimu, kwani linahusu uhai wa
dola yenyewe na siwezi kubeza. Hata hivyo, masuala kama Haki za Raia ni
muhimu zaidi kwani hata uwe na muundo wa namna gani wa Muungano au hata
Muungano wenyewe kuvunjika, bila ya kuwa na haki za msingi za raia,
katiba hiyo itakataliwa na wananchi.
Huu
mtindo unaozuka wa kudhani muundo wa Muungano ndio mwarobaini wa
matatizo ya ufisadi, matumizi mabaya ya madaraka, ubadhirifu, umasikini,
elimu ya hovyo, afya dhaifu, utatufikisha pabaya na hata kurudi tena
kuandika katiba kwa lengo la kudai haki hizo. Jaji Warioba na Rais
Kikwete wameshindwa kuruka kiunzi hicho na kutambua kuwa Katiba ni zaidi
ya Muungano.
Pili,
Rais Kikwete na Jaji Warioba wamejenga hoja zao kuhusu miundo ya
Muungano wanayopendekeza au kuunga mkono kutokana na misingi ama ya
'malalamiko' au 'hofu'.
Jaji
Warioba aliorodhesha malalamiko 11 ya upande wa Zanzibar dhidi ya
Muungano na malalamiko kumi ya upande wa Bara. Kimsingi malalamiko yote
ya upande wa bara yanazaliwa na vitendo vya upande wa Zanzibar,
isipokuwa lalamiko namba 'vii' linalohusu kupotea kwa utambulisho wa
Tanganyika katika Muundo wa Muungano.
Jaji
Warioba anajenga msingi wa pendekezo la tume yake kutokana na kujibu
malalamiko au maarufu kama kero za Muungano na anasema "Muundo wa
serikali mbili hauwezi kubaki kwa hali ya sasa. Muungano wa serikali
mbili waliotuachia waasisi siyo uliopo sasa... waasisi walituachia
Muungano wa nchi moja yenye serikali mbili, na siyo nchi mbili zenye
Serikali Mbili". Nukuu hii niliipenda kuliko zote katika Hotuba ya Mzee
wangu Warioba.
Rais
Kikwete alijenga msingi wa maoni yake kwenye hofu za kuwa na serikali
tatu. Hofu hizo ni pamoja na gharama za kuendesha Muungano, kuzuka kwa
hisia za utaifa wa Utanganyika na Uzanzibari, uwezekano wa Muungano
kuvunjika kwa kushindwa kuhudumia majeshi na hata Jeshi kuchukua nchi
ikibidi na kutupilia mbali katiba na Serikali ya Muungano kutokuwa na
Rasilimali zake.
Rais
alisema 'Serikali ya Muungano ni egemezi na tegemezi' nukuu ambayo
niliipenda kuliko zote katika Hotuba ya mzee wangu Kikwete.
Lakini
Rais hakuniridhisha kabisa namna ya kumaliza kero za Muungano kwa muundo
wa sasa kwani umeshindwa kuzimaliza kwa takribani miaka 50 tangu
Muungano uundwe.
Haiwezekani
muundo uliozalisha kero lukuki ndio utarajiwe kuzimaliza kero hizo. Kwa
vyovyote vile ni lazima kuwa na muundo mpya, lakini kiukweli ni lazima
muundo huo mpya ujibu hofu alizoeleza Rais maana ni hofu za kweli.
Naye Jaji
Warioba hakuniridhisha na namna suala la Uraia litakavyotatuliwa kwani
kutoa jibu la kubakia na 'kukubali' nchi mbili halafu uraia mmoja
kunatia shaka kubwa. Kama tunataka kuwa na Uraia mmoja ni lazima tuwe
nchi moja, hatuwezi kuwa na nchi mbili uraia mmoja.
Pia
vyanzo vya mapato ya Muungano ni vidogo mno kuendesha dola. Hivyo rasimu
iliyopo ina mapungufu makubwa japo imetoa mapendekezo yatakayomaliza
malalamiko.
Kazi ya Bunge sasa ni kuboresha rasimu ili kumaliza kero za Muungano na kuziondoa za hofu za muundo mpya.
Kama
kweli tunataka kusikia Watanzania wanataka nini kwenye muundo wa
Muungano, tusimamishe Bunge na twende tukawaulize kwa kura ya maoni.
Mwandishi wa makala haya ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini
CHANZO MWANANCHI.
No comments:
Post a Comment