Friday, February 7, 2014

Bunge la Katiba Februari 18, majina leo

Rais Jakaya Kikwete akisitiza jambo wakati akifungua mkutano wa Baraza la Vyama vya Siasa uliofanyika katika ukumbi wa mkutano wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam jana.
Rais Jakaya Kikwete jana alitangaza rasmi kuwa Bunge la Katiba litaanza  Februari 18, mwaka huu.
Aidha, alisema kuwa atatangaza majina ya wajumbe wa Bunge hilo leo.

Akizungumza kwenye kikao maalumu cha Baraza la Vyama vya Siasa jijini Dar es Salaam jana, Rais Jakaya Kikwete alisema maandalizi kwa ajili ya Bunge hilo yanaendelea vizuri na kilichobaki ni marekebisho madogo madogo.

“Wiki iliyopita nilitembelea kwenye ukumbi  wa Bunge la Katiba kwa kweli maandalizi yanaendelea vizuri, viti vimeshafungwa, na vipaza sauti vilikuwa vinafungwa na niliambiwa kuwa mpaka ifikapo Februari 10 (Jumatatu ijayo) kila kitu kitakuwa tayari,” alisema.

Aliongeza kuwa alishauriana na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na kwamba wamekubaliana kuwa Bunge hilo lianze Februari 18, ingawa sheria inawataka watangaze kuanza kwa kikao hicho cha Bunge hilo siku 21 baada ya kupokea Rasimu ya Katiba na Tangazo hilo bado halijawekwa rasmi, hivyo litatangazwa rasmi Februari 14.

Rais Kikwete aliongeza kuwa Bunge hilo linatarajiwa kuchukua siku 70, lakini lisipomaliza kazi yake kwa muda uliopangwa litaongezewa siku nyingine 20 ili liweze kumaliza kazi yake.

Alisema wananchi walioomba nafasi ya kuwa wajumbe wa baraza hilo ni 3,774 na wanaotakiwa ni 201 na wale walioomba kutoka mashirika mbalimbali ni 1,647 wakati nafasi zilikuwa ni 20.

Aliendelea kufafanua kwamba wajumbe walioomba kutoka Taasisi za Dini walikuwa 329 wakati nafasi zilikuwa ni 20 tu, walioomba kwa kupitia vyama vya siasa walikuwa ni 198 wakati nafasi zilikuwa ni 42, walioomba kutoka Taasisi za Elimu ni 130, huku nafasi zikiwa ni 20.

Walioomba kutoka makundi ya walemavu ni 140 huku nafasi zikiwa ni 20, walioomba kutoka vyama vya wafanyakazi ni 102 wakati nafasi zilikuwa 19, kutoka makundi ya wafugaji 47 wakati nafasi zikiwa ni 10, makundi ya wavuvi ni 57 wakati waliotakiwa ni 10 na makundi ya wakulima ni 157 wakati nafasi zilikuwa ni 20.

“Makundi yenye mrengo unaofanana walikuwa 127 wakati waliochaguliwa ni 10, hivyo watu 3,593 hawatakuwamo ila siyo kwamba hawafai, kwani ukiangalia sifa zao ni wasomi na wana uzoefu,” alisema.

Alisema wengi kati ya watu walioomba walikuwa na sifa na vigezo pamoja na elimu stahiki, lakini ilikuwa ni lazima wapatikane wachache kwa kuzingatia nafasi zilizopo na kwamba wale waliokosa hawakukosa kwa kukosa sifa.

Hata hivyo, Rais Kikwete aliwaasa viongozi na wajumbe wa vyama vya siasa kuweka kando maslahi yao na ya vyama vyao na kuweka maslahi ya Taifa mbele ili kuhakikisha inapatikana Katiba mpya kwa wakati na unaofaa.

Vilevile, alisema bunge hilo ndilo lenye mamlaka ya kupitisha rasimu hiyo na kuwa Katiba, hivyo wajumbe hao wajue wana dhamana kubwa kwa wenzao katika kuipatia nchi katiba nzuri na itakayodumu kwa muda mrefu hata kwa miaka 50 ijayo, ambayo itadumisha Muungano, amani, mshikamano uchumi na maendeleo kwa wananchi.

Rais Kikwete aliwataka wajumbe wa Bunge hilo wajue kinachojadiliwa ni  vile vinavyofaa na visivyofaa, na kwamba vyama vya siasa vina nafasi kubwa sana kwa kuwa Bunge hilo lipo chini ya vyama vya siasa.

“Kufanikiwa kwa Bunge hilo kutatokana na vyama vya siasa, sasa msipoelewana ninyi basi na kule hakuna litakaloeleweka, kufanikiwa kunatokana na ninyi na wanachama wenu, na ndiyo mtakaojenga au kubomoa, mimi nataka mjenge na siyo kubomoa” alisema na kuongeza:

“Tupate Katiba mpya kwa wakati ili ituwezeshe kwenye uchaguzi ujao, mimi naamini vyama vikishirikiana katiba itapatikana bila ya kelele kama vyama vitatambua kuwa tunatengeneza jambo la  wote na siyo la vyama vyao.”

“Hatuendi kule kutengeneza katiba ya CCM, Chadema wala ya NCCR, hilo tukilikamilisha tutakuwa tumevuka kikwazo cha kwanza, kama vyama vitakubali kuongozwa kwa nguvu za hoja watakazotoa wajumbe na siyo nguvu ya hoja ya mjumbe,” alisema Kikwete.

Akisisitiza wajumbe hao kuacha kupinga kila hoja ambayo inatolewa na mtu kwa kuwa tu mtu huyo anatoka chama fulani, na kuunga mkono yale tu yanayotolewa na wajumbe wa chama chake hata kama mtu huyo hana hoja ya msingi.

Aliwataka kuwa tayari kusikiliza maoni ya hata wale wasiowapenda, ili mradi yawe na maana na hoja za msingi kwani ni haki ya kila chama kutoa maoni yao, lakini waende na maoni hayo kama maoni na siyo amri, na hata pale watakapoitana na kuelezana msimamo wa vyama vyao kwa wenzao hilo halina shida.

Aliongeza kuwa ni vyema viongozi wa siasa kwenda kwenye Bunge hilo huku wakiwa na lengo la kuwasikiliza wengine, na mchakato wa katiba hiyo utafanikiwa kwani watu watatofautiana kwa hoja tu na siyo itikadi za vyama vyao.

“Ni vyema tukawa na katiba inayojali maslahi ya Watanzania ndani na nje ya muungano, anakoishi na ndani ya historia yake,” alisisitiza Rais Kikwete.

Aliwaambia viongozi hao wa vyama vya siasa kwama wasipokuwa makini wataivuruga nchi, na kutengeneza lindi la la uadui na kuleta chuki miongoni mwa wananchi.

MUUNGANO, UKOMO UBUNGE
Pia alivitaka vyama hivyo kushirikiana kwenye mijadala migumu zaidi ya mjadala wa mfumo upi ufuatwe kwenye Muungano, ambayo ni ule wa serikali mbili au serikali tatu.

“Kuna mambo magumu kwenye rasimu kwani hata sisi tulipokuwa tunajadili rasimu hiyo tuligundua mambo magumu, kama kile kipengele kinachosema kuwa mtu akiwa ameshakuwa mbunge kwa vipindi vitatu anapoteza sifa za kuwa mbunge,” alisema.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alisema: “Tanzania ni yetu sote, na ni zaidi ya siasa, hivyo ni vyema tukawa makini katika yale tunayotenda kuliko kusema na kutenda tofauti na tunayosema kwani wananchi wanataka katiba itakayagusa maisha yao.”

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendelao (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, alisema Rais Kikwete hajagusia jinsi gani watazingatia maoni ya wananchi katika kuijadili rasimu ya katiba hiyo.

Katika mkutano huo viongozi wa vyama vyote 21 vyenye usajili wa kudumu walihudhuria na vingine vilituma wawakilishi wao.

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kiliwakilishwa na Katibu Mkuu, Abdulrahman Kinana; Makamu Mwenyekiti Bara, Philip Mangula; Dk. Asha-Rose Migiro,  ambaye ni Katibu Siasa na wa Mambo ya Nje na Naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Vuai Ali Vuai.

Chadema kiliwakilishwa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe na Dk. Slaa na Katibu Ofisi ya Katibu Mkuu ya chama hicho, Victor Kimesera.

Pia alikuwapo Mwenyekiti wa UDP, John Cheyo, Mwenyekiti wa Chausta, James Mapalala na Peter Kuga Mzirai ambaye ndiyo Mwenyekiti wa Baraza hilo.

Bunge hilo linaundwa na wajumbe 635 ambao ni 358 kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, wajumbe 76 kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar na wajumbe 201 kutoka mashirika yasiyo ya serikali pamoja na taasisi za kidini.
 
CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment