
Dodoma. Rasimu za kanuni za uendeshaji
Bunge Maalumu la Katiba zimependekeza kutumika kwa utaratibu wa kupiga
kura ya siri wakati wa kupata uamuzi wa kupitisha Rasimu ya Katiba.
Endapo mapendekezo hayo yatapitishwa,
hoja ya Katiba Mpya itakayowasilishwa na Kamati ya Bunge Maalumu la
Katiba, itaamuliwa kwa kuungwa mkono na theluthi mbili ya wajumbe wa
Tanzania Bara na idadi kama hiyo ya wajumbe kutoka Tanzania Zanzibar
.
Upigaji kura huo kwa siri, umepongezwa
na baadhi ya wabunge kwa maelezo kuwa utatoa fursa kwa wajumbe kupiga
kura hizo kwa uhuru na bila kushinikizwa na misimamo ya vyama au taasisi
zilizowapendekeza.
Kanuni hizo zimekuja wakati CCM,
kikiwa kimewaagiza wajumbe wake ambao ndiyo wengi bungeni, kutetea
muundo wa Serikali mbili badala ya ule wa Serikali tatu uliopendekezwa
na Tume ya Mabadiliko ya Katiba iliyoongozwa na Jaji Joseph Warioba.
Pamoja na CCM kuweka msimamo wa
kuwataka wajumbe wake kuutetea mfumo huo, kumeibuka mgawanyiko mkubwa
huku baadhi yao wakitarajiwa kukitosa na kuunga mkono mfumo wa Serikali
tatu.
Kanuni ya 82(1) ya rasimu hiyo,
imeweka bayana kuwa utaratibu utakaotumika kupata uamuzi baada ya
mwenyekiti kulihoji Bunge ni wa ama kura ya siri au ya kielektroniki.
"Wakati wa kupiga kura ya siri, kila
mjumbe atapiga kura ya Ndiyo au Hapana kwa kutumia karatasi za kupigia
kura zitakazokuwa zimeandaliwa na Katibu wa Bunge," inasomeka kanuni ya
83(1).
Kanuni hiyo imeweka wazi kuwa kupiga
kura kwa mujibu wa masharti ya kanuni hiyo, itakuwa ni wajibu na haki ya
msingi ya kila mjumbe na kwamba kila mjumbe atapiga kura kwa binafsi
yake.
Hatua ya wajumbe kupiga kura hiyo,
itatanguliwa na kazi ya kila Kamati ya Bunge Maalumu, kujadili rasimu ya
katiba hiyo kulingana na mgawanyo wa majukumu. Kamati 17
zitashughulikia ibara za rasimu.
Baada ya kukamilika kwa hatua hiyo,
mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ataagiza taarifa ya kamati iwekwe kwenye
orodha ya shughuli kwa ajili ya kuwasilishwa bungeni kwa mjadala.
Kanuni hizo zimeeleza kuwa wakati wa
mjadala huo, mjumbe yeyote anaweza kushauri na kutoa mapendekezo ya
marekebisho au mabadiliko kwa ajili ya kuboresha sura ya rasimu
inayohusika.
Hata hivyo, Kanuni za 78 (11) na 78
(12) za rasimu hiyo, zinapendekeza mwenyekiti asiruhusu hoja yoyote
inayokiuka sheria au pendekezo la kamati linalohusu jambo lililo nje ya
mamlaka ya Bunge.
Rasimu hizo za kanuni zimegawanywa kwa
wajumbe wote 629 wa Bunge Maalumu la Katiba na kuanzia juzi hadi
Jumapili, watakuwa wakizisoma na baadaye kuanza kujadiliwa Jumatatu
ijayo.
Akizungumzia upigaji kura kuwa wa
siri, Mjumbe wa Bunge Maalumu, Grace Kiwelu alisema utaratibu huo utatoa
fursa kwa wajumbe kuwa huru kufanya uamuzi wenye masilahi kwa taifa
badala ya vyama.
Mjumbe mwingine, Esther Bulaya naye
alisema kanuni hiyo ni mwafaka kwa sababu itawafanya wabunge kupiga kura
kwa uhuru na bila kuhofia kwamba chama au taasisi iliyompendekeza
inamtazama.
"Ifahamike kuwa utungaji wa Katiba ni
zaidi ya vyama vya siasa... hii ni Katiba ya Watanzania wote na kura ya
siri itawafanya wajumbe wawe huru kufanya uamuzi kwa masilahi ya umma wa
Watanzania," alisema. Bulaya alikosoa mfumo wa kura ya wazi unaotumika
katika Bunge la Jamhuri, akisema unamfanya mpigakura kushindwa kutumia
utashi wake kufanya uamuzi sahihi akihofu kushughulikiwa na chama chake.
source: Na Daniel Mjema, Mwananchi
No comments:
Post a Comment