Tuesday, May 21, 2013

Tukichoka kuhubiri amani, tujiandae na kazi ya kuchimbiana makaburi - Maggid Mjengwa

Ndugu zangu,

Naiona hatari kubwa nyingine inakuja mbele yetu. Ni haya makundi mawili; MaBodaboda na MaMachinga. Hofu yangu kuna wanasiasa wachache wanaowaona vijana hawa, katika matatizo yao ya kiuchumi, kuwa ni mtaji wa kisiasa. Na kimsingi wanawageuza kuwa ' Shuka za Kisiasa'. Na hapa ni wanasiasa wa vyama vyote.

Hatari yake?
Viongozi wasipokuwa makini, wakaacha kutanguliza busara na hekima kwenye kauli zao, basi, hofu ya kauli kupelekea machafuko na kuvunjika kwa amani itabaki kuwepo.

Maana, hawa MaBodadoba na MaMachinga, pamoja na kuwa wengi wao ni vijana wema kabisa, na ambao, kwenye mahangaiko yao, kama wagonjwa, wanamsikiliza kila anayekuja na kauli za kuwapa matumaini, hata kama ni ya muda mfupi,  na hata kama ni kwa kuvunja sheria.

Na kwa vile Elimu ya Uraia iko chini sana katika jamii yetu, hata kwa miongoni mwa viongozi wetu, basi, ndio maana naiona hatari hii kubwa inayokuja mbele yetu. Kwamba MaBodaboda na MaMachinga wakiendelea kutumiwa kama ' Shuka za Wanasiasa', basi, yumkini, huko tuendako Watanzania tujiandae na kazi ya kuchimbiana makaburi.

Maana, siku zote, maovu huzaa maovu. MBodaboda au Mmachinga mmoja akiuawa, kuna mia watakaokuja kutaka kulipiza kisasi. Na Polisi mmoja akiuawa, kuna operesheni ya kipolisi itakayofuata. Na polisi wetu hawa ni vijana hawa hawa ambao wengine wameponea chupuchupu kuwamo  kwenye makundi haya ya MaBodaboda na MaMachinga, lakini sasa, tumewapa pia silaha za moto wabebe.

Naam, tukichoka kuhubiri Amani, Upendo Na Mshikamano, basi, tujiandae na kazi ya kuchimbiana makaburi.

Maggid
Iringa

No comments:

Post a Comment